Rais wa Marekani, Donald Trump, amezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoa kauli kuhusu umbo la rapa maarufu Nicki Minaj wakati wa mkutano wa kampeni za Chama cha Republican uliofanyika Port Huron, Michigan, Jumapili,
Trump alitoa kauli hiyo alipokuwa akilihutubia kundi la wafuasi wake, kabla ya kumkaribisha Minaj jukwaani, ambapo alimsifia kwa maneno yaliyosababisha umati wa watu kushangilia.
Akizungumza mbele ya wafuasi wake, Trump alirejelea maoni yake ya awali kuhusu umbile la Seneta wa Republican kutoka Ohio, Jon Husted, kabla ya kuhamishia mazungumzo yake kwa Minaj.
“Kwa njia, nililitazama umbo moja la kuvutia sana hapo awali Nicki Minaj,” alisema Trump, kauli iliyopokewa kwa shangwe na umati. Baadaye alimtaka rapa huyo kusimama na kuongeza kuwa ni vigumu kutomwona.
Trump pia alieleza matumaini yake kuwa Minaj hakuudhika na kauli hiyo, akisisitiza kuwa anampenda na kwamba rapa huyo amekuwa akimuunga mkono kwa muda mrefu.
Baada ya Minaj kumaliza kuzungumza na hadhira, Trump aliendelea kumsifia, akisema ni mrembo zaidi na mwanamke mwenye akili.
NICKI MINAJ ATOA SAPOTI KWA TRUMP
Minaj, mwenye umri wa miaka 43, alitumia nafasi yake katika mkutano huo kueleza wazi kumuunga mkono Trump, huku akiwa amevalia suti ya rangi ya dhahabu yenye nembo ya Gucci.
Akizungumza jukwaani, alisema anajivunia kufanya kazi na Rais huyo, akimtaja kama kiongozi anayewakilisha uvumilivu na uwezo wa kusimama tena baada ya changamoto.
Rapa huyo aliongeza kuwa kurejea kwa Trump madarakani kumebadilisha hali ya nchi na kuwapa Wamarekani matumaini mapya kwa ajili yao na watoto wao.