Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameahidi kutoa mtaji kwa vijana wa Kitongoji cha Ipilinga, Kata ya Kisuke, Halmashauri ya Ushetu, ili kuanzisha kikundi cha ujasiriamali cha kufyatua matofali yatayotumika kuboresha makazi ya wananchi.
Mboni amesema mpango huo utasaidia kuongeza ajira na kipato kwa vijana, huku ukichangia upatikanaji wa matofali kwa wananchi na kuboresha ujenzi wa nyumba imara katika kitongoji hicho.
Ametoa ahadi hiyo katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Ipilinga, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Wilaya ya Kahama.
Amesema mradi atakaoufadhili utahusu utengenezaji wa matofali ya kuchoma ambayo yanatumia nishati isiyohusisha ukataji miti wakati wa kuyaandaa.
“Kuna uboreshaji umefanyika kwenye matofali ya kuchoma sio lazima ukate miti. Mimi najitolea, kuna Mkurugenzi wa Halmashauri hapa, Ofisa Maendeleo ya Jamii yupo…nahitaji kikundi kimoja hapa cha vijana.
“Moja kati ya kazi watakayofanya, waandikiwe mradi wa ufyatuaji wa matofali yenye ubora ya kuchoma kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa.
“Mahitaji ya awali watakayohitaji, naomba mniambie…mimi nitafadhili mradi huu kuhakikisha kwamba Kitongoji chetu tunakwenda kukibadilisha kwa ujenzi wa kisasa na matofali ya kisasa,” amesema Mboni.
Amewahimiza wakati wa Kitongoji hicho kuanza ujenzi wa nyumba za kisasa ili kubadili taswira ya makazi yao.
“Vijana changamkieni fursa, mtaji wa kuhakikisha huo mradi tunauanzisha na kuuinua kabisa nimeahidi nitasaidia, ili tuhakikishe kwamba ndani ya Kitongoji chetu tuna vijana mahiri wa ufyatuaji wa matofali. Mnaenda kuwa suluhisho na waokoaji wakubwa wa maisha ya watu,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa za El-Nino zinazotarajiwa kunyesha, hivi karibuni ikiwemo kuimarisha nyumba na miundombin,u ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.