Wakazi 344 kati ya 346 waliofika kwenye zoezi la tathmini, katika Mtaa wa Mgeo Kata ya Buhanda, Manispaa ya Kigoma, wameridhia fidia zao na kusaini fomu za kuthibitisha uhakiki wa taarifa zao za mali zinazohusika na mradi wa reli ya kisasa (SGR).
Hayo yameelezwa leo na Mthamini Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rashid Mageta, huku akibainisha kuwa wakazi hao ni sehemu ya wananchi 370 waliofanyiwa thamini katika eneo hilo.
Amesema hadi sasa wakazi 346 wamefika kuhakiki taarifa zao, huku 344 wakiridhia fidia na kusaini fomu za uhakiki, ambapo ni wakazi wawili pekee ambao hawajaridhishwa na fidia walizoainishiwa.
“Mpaka sasa wananchi 344 wameridhia fidia na kusaini fomu za uhakiki wa taarifa zao na awili hawakuridhia fidia hiyo. Vilevile, wakazi 24 kati ya 370 waliofanyiwa uthamini bado hawajafika kuhakiki taarifa zao,” amesema Mageta.
Amesema zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini ya Mwaka 2018 na kanuni zake, huku akitoa wito kwa wakazi 24 ambao hawajafika kuhakiki wa taarifa zao na kutoa hoja.
Mageta amesisitiza kuwa ushiriki katika zoezi la tathmini ni hatua muhimu katika mchakato wa uthamini, kwa kuwa humpa mwananchi fursa ya kuona na kuhakiki taarifa za mali yake pamoja na taarifa zinazohusiana na fidia.
Ameongeza kuwa wananchi wanaohusika wanapaswa kutumia fursa hiyo kuhakiki taarifa zao na kutoa hoja kwa wakati, hatua inayosaidia kubaini na kushughulikia changamoto mapema kabla ya kukamilika kwa mchakato wa uthamini na ulipaji wa fidia.
Aidha, amewahimiza wakazi 24 ambao bado hawajahakiki taarifa zao na kushiriki kabla ya hatua zinazofuata za mchakato wa mradi wa SGR.
Mmoja wa wakazi wa Mgeo aliyeridhia fidia hiyo, John Samizi, amesema mchango wa uthamini wa maeneo yao umekwenda vizuri na kufikia muafaka wa kupisha mradi huo, ambapo kwa sasa wako kwenye hatua za kusaini nyaraka, ili kuhama eneo hilo.
“Tunashukuru serikali imefanya uthamini wa eneo letu na mali tunazomiliki ikiwemo ardhi, nyumba na mali zingine na wametuelekeza vizuri namna ya kupata stahiki zetu. Ni jambo zuri kuwa eneo letu litatumika kwa ajili ya mradi mkubwa wa taifa letu,” amesema Samizi.