Hali ya kibinadamu Yemen inazorota haraka baada ya kuongezeka kwa mapigano. Wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi.
Mashambulizi mapya ya anga na mapigano makali nchini Yemen yameongeza hofu ya kurejea kwa vita vikubwa, huku maelfu wakikimbia makazi yao. Hali ya kibinadamu inazidi kuzorota haraka huku wanawake na watoto wakiathirika zaidi. Mashirika ya misaada yanaonya juu ya janga hilo la kibinadamu linaloongezeka.
Milipuko mikubwa ilisikika Alhamisi usiku katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, baada ya mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.
Mashuhuda waliliambia shirika la habari la dpa kwamba moshi ulionekana ukifuka karibu na ikulu ya rais na eneo la mlima Al-Nahdain. Kituo cha televisheni cha Wahouthi, Al-Masirah, kilisema mashambulizi hayo yalilenga Sanaa pamoja na majimbo ya Saada, Taiz na Amran.
Hatua hiyo ilifuatia tangazo la Saudi Arabia kwamba ilizuia makombora mawili na ndege nne zisizo na rubani zilizorushwa na Wahouthi kuelekea maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.