Watanzania wamehimizwa kuzingatia mlo kamili na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya ya mifupa na viungo pamoja na kupunguza hatari ya kupata matatizo yanayohusiana na mifupa na viungo.
Wito huo umetolewa na Fiziotherapisiti George Claud kutoka Garma Specialized Physiotherapy Clinic iliyopo jijini Mwanza, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Afya ya Mifupa na Viungo kwa Watoto, Oktoba 19, 2026.
Akizungumzia umuhimu wa lishe, George amesema mlo kamili una nafasi kubwa katika kuimarisha afya ya mwili, akisisitiza ulaji wa vyakula vyenye virutubisho muhimu ikiwemo madini ya kalsiamu, Vitamini D kupitia Mwanga wa jua la Asubuhi na vyakula kama mayai, samaki na mboga za majani vinasaidia kuimarisha mifupa.
"Tunapaswa kuzingatia namna bora ya ulaji kwa kuhakikisha chakula kinajumuisha makundi mbalimbali, kama vile wanga, protini na vitamini. Mtu anayefanya kazi ngumu anahitaji kupata chakula chenye wanga na protini kulingana na mahitaji ya mwili. Protini husaidia kujenga mwili na ukuaji wa watoto, wanga hutoa nishati, huku vitamini zikisaidia kulinda afya ya mwili. Ni vyema kuzingatia makundi ya chakula badala ya kula kwa mazoea," amesema George.
Aidha, amesema mazoezi yana nafasi muhimu katika kuimarisha afya ya mifupa na viungo, akiwataka watu wa rika zote kufanya mazoezi yanayolingana na uwezo wao wa kiafya na kuzingatia ushauri wa wataalamu.
"Kwa upande wa mazoezi, tunashauri mtu kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30, kulingana na uwezo wake na ushauri wa wataalamu wa afya. Kufanya mazoezi bila kuzingatia hali ya mwili na ushauri wa kitaalamu kunaweza kusababisha madhara, hivyo ni muhimu kila mtu kufanya mazoezi yanayolingana na umri na hali yake ya kiafya," amesema George.
Akizungumzia dalili zinazoweza kuashiria matatizo ya mifupa na viungo, George ametaja maumivu makali ya viungo ya muda mrefu muda mwingine yakiambatana na uvimbe, maumivu ya Mgongo na miguu, akiwashauri wananchi kufika katika vituo vya Afya pale wanapokumbana na dalili hizo.
Ameongeza kuwa namna ya ukaaji inapaswa kuzingatiwa kwa kuepuka kukaa kwa muda mrefu, kutofanya mazoezi na kutoupa mwili shughuli za kimwili, akieleza kuwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ni muhimu kwa afya ya mifupa na viungo.
Katika hatua nyingine, George amesema baadhi ya matatizo ya mifupa na viungo yanaweza kutibika hata kwa wazee, kutegemea aina ya tatizo na hali ya mgonjwa, akisisitiza umuhimu wa kuwahi kupata huduma sahihi ikiwemo tiba ya viungo inapohitajika.
Amewasisitiza wananchi kupima afya zao mara kwa mara, kuzingatia mlo kamili na kufanya mazoezi kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kudumisha afya bora ya mifupa na viungo.
Imeandikwa| Martin Mbilinyi