Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amependekeza kufanyika kwa mkutano wa kilele mwezi ujao akishirikiana na Rais wa Marekani, Donald Trump, na Rais wa China, Xi Jinping, kwa lengo la kujadili makubaliano ya kumaliza vita vya Ukraine vinavyoendelea kwa mwaka wa nne, kwa masharti yanayoinufaisha Moscow.
Kwa mujibu wa gazeti la The Wall Street Journal (WSJ), likinukuu watu wanaofahamu mazungumzo hayo, pendekezo hilo lilitolewa na Putin wakati wa mazungumzo yake kwa njia ya simu na Trump Oktoba 9, mwaka huu.
Pendekezo hilo linakuja wakati uhusiano kati ya Trump na Putin ukiendelea kuimarika, hasa baada ya Rais huyo wa Marekani kutangaza makubaliano ya kununua dizeli kutoka Urusi na kusaini agizo la kuondoa kwa muda baadhi ya vikwazo muhimu vilivyowekwa dhidi ya Moscow.
WSJ limeripoti kuwa Kremlin imependekeza mazungumzo hayo ya viongozi hao watatu yafanyike pembezoni mwa mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC), unaotarajiwa kufanyika Novemba 18 hadi 19, mwaka huu, jijini Shenzhen, China.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amethibitisha kwa gazeti hilo kuwa majadiliano kuhusu uwezekano wa mkutano huo yanaendelea, ingawa bado hakuna uamuzi wa mwisho kuhusu kufanyika kwake au ajenda itakayojadiliwa.
“Hakuna uelewa wa wazi kuhusu mkutano wenyewe au ajenda yake inayoweza kujadiliwa, ingawa pande zote tatu zinatambua uwezekano wa mkutano huo kufanyika,” Peskov alinukuliwa akisema.
Hata hivyo, afisa mmoja mwandamizi wa Marekani ameliambia WSJ kuwa Trump bado hajakubali kushiriki mkutano huo, ingawa anaweza kulipokea vyema pendekezo hilo.