Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, ametangaza tarehe 19 Oktoba kuwa ameamuru wakuu wa mikoa kutangaza sheria ya kutotoka nje katika baadhi ya maeneo na za muda kuanzia usiku wa kuamkia leo, kwa lengo la kulinda maduka na maeneo mengine kutokana na ghasia na wizi vilivyotokea mwishoni mwa wiki hii iliyopita. Hata hivyo, serikali haikujibu madai ya waandamanaji, huku vuguvugu la "vizibao vya njano" likitoa wito kwa siku nyingine ya maandamano Jumamosi, Oktoba 24.
Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, amesisitiza leo Jumatatu kwamba hali ya hatari inaweza kutangazwa "ikiwa ni lazima," huku akionya kuwa suala hilo sio " la kisiasa" na kwamba utekelezaji wa sheria ya kutotoka nje usiku unaonekana kwake kuwa "unafaa zaidi." Mkuu wa serikali anaacha mlango wazi kwa hatua ambayo ilikuwa imetakiwa na mrengo wa kulia na mrengo wa kulia wenye msimamo mkali.
"Azimio langu la kurejesha utulivu ni kamili," amesema Sébastien Lecornu baada ya mkutano wa dharura wa mawaziri. Hali ya dharura, "ni hatua ngumu sana, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wake. Kwa hivyo ikiwa ni lazima, bila shaka tunaweza kuifanya. Kwa hali ilivyo, suala la sheria ya kutotoka nje, utekelezaji wake, kwangu mimi linaonekana linafaa zaidi kwa hali ya sasa", amesema Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sébastien Lecornu.
Hayo yanajiri wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikemea vikali kile alichokiita ghasia "zisizo na kikomo" zilizozuka wakati wa maandamano dhidi ya gharama ya maisha kote nchini humo mwishoni mwa wiki.
Takriban waandamanaji 550,000 waliingia mitaani katika maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani, kupinga kupanda kwa bei ya mafuta, gharama ya maisha, na kuzorota kwa huduma za umma, ikiwemo shule.
Katika hotuba kwa taifa Jumapili usiku akiwa Ikulu ya Elysée, Macron aliapa kuwa serikali ya Ufaransa itawakabili vilivyo "wachochezi kutoka makundi ya msimamo mkali wa mrengo wa kushoto, waliojumuika na wahalifu wengi," ambao "walizua vurugu zisizo na kikomo mijini."