MAANDALIZI ya kuanza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha kampuni ya Dangote katika Kaunti ya Lamu yameshika kasi, huku wakazi wakizidisha wito wa kutaka kushirikishwa kikamilifu na kutatuliwa masuala ya fidia za miradi mikubwa ya zamani.
Jumatatu, wajumbe wa Kenya wakiongozwa na Rais William Ruto, walikutana na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote, ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Dangote Industries, pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Amerika.
Rais Ruto alisema Kenya iko tayari kuanza rasmi ujenzi wa kiwanda hicho cha ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumejitolea kuhakikisha mradi huu wa kihistoria unatekelezwa huku tukihakikisha unaleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi,” alisema Dkt Ruto.
Jumanne, Naibu Rais Kithure Kindiki alithibitisha kuwa hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa mradi huo imepangwa kufanyika Septemba 30.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Prof Kindiki alisema maandalizi ya hafla hiyo yanaelekea kukamilishwa ili kuhakikisha inaendeshwa kwa hadhi inayostahili.
Naibu Rais alisema viongozi wa nchi za ukanda huu wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo pamoja na jamii za Lamu.
“Tuna matumaini makubwa kwamba mradi huu utatusaidia kuunda nafasi za ajira 50,000 katika eneo hili. Pia tunafurahia kwa sababu mradi huu utawezesha jamii za Lamu na eneo la Pwani kupitia uundaji wa ajira na fursa nyingine,” aliongeza.
Wiki iliyopita, Rais Ruto alisema shughuli za ujenzi wa kiwanda hicho na bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Lokichar hadi Lamu huenda zikaendelea kwa wakati mmoja.
Kauli hiyo ilizua malalamiko miongoni mwa wakazi wa Lamu wanaodai kuwa, bado kuna masuala ya fidia ambayo hayajatatuliwa kuhusu ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya mradi wa bomba hilo, huku wakitaka uwazi kuhusu mipango ya kiwanda hicho.
Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari katika Ikulu ya Kisumu, Rais Ruto alisema serikali inashauriana na Dangote Group kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Turkana.
Wakazi kupitia Chama cha Wakulima wa Kililana, kundi la kijamii linalowawakilisha wamiliki wa ardhi na wakazi wanaoishi hasa katika maeneo yanayopakana na sehemu za mradi wa Uchukuzi kati ya Bandari ya Lamu-South Sudan-Ethiopia (LAPSSET), wamehoji kwa nini mipango inaonekana kuendelea kwa kasi huku masuala muhimu yanayoathiri jamii yakiwa bado hayajatatuliwa.
Katibu wao, Bw Mohamed Rajab, alitoa wito wa ushirikishwaji wa umma ili kutatua masuala ya fidia kabla ya hatua nyingine za mradi huo kuendelea.
Bw Rajab alihoji kwa nini hadi sasa serikali imeendelea kuwa kimya kuhusu eneo ambako kiwanda cha mafuta cha Dangote kitajengwa Lamu.
“Kwa nini serikali inawaacha wenyeji gizani kuhusu eneo halisi ambako kiwanda hiki kinachokusudiwa kitajengwa? Kwa nini ratiba inaendeshwa kwa haraka? Hakuna mtu ambaye amekuja kutueleza eneo hilo liko wapi,” alisema Bw Rajab.
Aliongeza kuwa bado kuna masuala ambayo hayajatatuliwa kuhusu ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba katika miaka iliyopita. “Ardhi yetu ilichukuliwa na hatukufidiwa. Tutatafuta haki mahakamani kuhusu masuala haya yote,” alisema.
Bw Mbwana Shee, Mwenyekiti wa Shungwaya Welfare Association, shirika la kijamii linalotetea haki za ardhi za jamii ya asili ya Bajuni huko Lamu, alielezea masikitiko kwamba kila mara serikali inapopanga kuwekeza katika mradi mkubwa kaunti hiyo, wenyeji huachwa nje ya maamuzi yanayogusa moja kwa moja maisha na riziki zao.
Bi Raya Famau, mwanaharakati wa mazingira na Mkurugenzi Mkuu wa Lamu Women Alliance, aliitaka serikali kuhakikisha kunakuwa na mashauriano ya uwazi na jamii zote zilizoathirika.