Ubelgiji na Rwanda zimetangaza kukubaliana kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia, hii ikiwa ni hatua ya kuanza kurekebisha uhusiano ulionekana kuvunjika mwaka uliopita kutokana na mzozo wa DRC.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo, mataifa hayo sasa yanatarajiwa kufungua tena balozi zake jijini Kigali na Brussels.
Uhusiano kati ya mataifa hayo uliingia dosari mwaka uliopita baada ya Ubelgiji kuikosoa Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wakati wa uvamizi wao mashariki mwa DRC.
Kigali ilikatisha ushirikiano wake na Brussels mwezi Machi mwaka jana na kuwafukuza wanadiplomasia wa Ubelgiji, Kigali ikidai Brussels imekuwa ikiingilia masuala yake ya ndani mara kwa mara.
Katika taarifa yao ya pamoja, zimesema uamuzi wao unatokana na majadiliano na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya mawaziri wa mambo ya nje, ambapo masuala tata na yaliyokuwa hayajaeleweka na pande hizo yalipatiwa ufumbuzi.
Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda ilichapisha picha ya Waziri wake Olivier Nduhungirehe akisalimiana na mwenzake wa Ubelgiji Maxime Prevot nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.