Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, Jumanne ya wiki hii alitangaza kulivunja bunge la nchi nchi hiyo na kuteua utawala wa mpito, hatua aliyoichukua wakati huu taifa hilo likijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwezi Desemba mwaka huu.
Tangazo hili limekuja siku moja kupita tangu wabunge wapitishe sheria ambayo iliwafuta kazi manaibu wawili wa Rais na kumfanya Kiir abaki mwenyewe madarakani, uamuzi ambao wachambuzi wa mambo wanasema unampa madaraka makubwa zaidi kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa tangazo lililosomwa kupitia televisheni ya taifa, manaibu rais, mawaziri na viongozi wa serikali za mitaa wataachia nafasi zao isipokuwa kwa wale vyombo vya usalama na mahakama.
Kwa baadhi ya watu, uamuzi huu unaondoa moja ya kizuizi kikubwa kilichokuwepo kwa nchi hiyo kufanya uchaguzi mkuu wake wa kwanza baada ya kuahirishwa kwa zaidi ya mara mbili, uchaguzi wa mwaka huu ukitarajiwa kufanyika Desemba 22.
Aidha hatua hii imefikiwa huku kukiwa na hofu ya nchi hiyo kurejea kwenye machafuko, hasa kutokana na kuendelea kushikiliwa kwa aliyekuwa makamu wa kwanza wa rais na hasimu mkubwa wa rais Kiir, Riek Machar anayeshtakiwa kwa makosa ya uhaini.