LANGO JIPYA LA BIASHARA UKANDA WA MAZIWA MAKUU

Kigoma ni mwisho wa reli.” Ingawa ulitamkwa kwa utani, kwa kiasi kikubwa uliakisi hali halisi ya miundombinu na mtazamo uliokuwepo kuhusu mkoa huo. Wengi waliiona Kigoma kama eneo la mwisho wa safari badala ya lango la biashara na uchumi. 

Licha ya kuwa na Bandari ya Kigoma katika Ziwa Tanganyika na kupakana na masoko makubwa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Zambia, uwezo wake wa kuchochea biashara ya kikanda ulikuwa mdogo kutokana na changamoto za miundombinu ya usafirishaji. 

Gharama kubwa za kusafirisha mizigo, safari ndefu na kutokuwepo kwa mfumo wa kisasa wa uchukuzi vilifanya fursa nyingi za kiuchumi zibaki bila kutumika ipasavyo.

Hata hivyo, taswira hiyo inaanza kubadilika kupitia mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwekeza kwa wakati mmoja katika Reli ya Kisasa (SGR), bandari, usafiri wa majini, viwanja vya ndege na huduma nyingine za msingi. Badala ya kutekeleza miradi kama miradi ya kawaida ya maendeleo, Serikali imejenga mfumo jumuishi wa miundombinu unaolenga kuifanya Kigoma isiwe tena mwisho wa safari, bali lango la biashara, usafirishaji na uwekezaji litakalounganisha Tanzania na ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na Kusini mwa Afrika.

Mkakati huo unaendana na maono ya muda mrefu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka msisitizo katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa kama msingi wa kukuza uchumi shindani, kuongeza tija katika uzalishaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji barani Afrika. Dira hiyo inabainisha kuwa reli za kisasa, bandari, viwanja vya ndege, barabara na usafiri wa majini ni nguzo muhimu za kuunganisha masoko ya ndani na ya kikanda, kupunguza gharama za usafirishaji na kuvutia uwekezaji. 

Kwa muktadha huo, uwekezaji unaoendelea mkoani Kigoma haupaswi kutazamwa kama mradi wa maendeleo ya mkoa mmoja pekee, bali kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kujenga uchumi unaounganishwa na masoko ya Afrika Mashariki, ukanda wa Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii