Rebeca Grynspan wa Costa Rica ameongoza duru ya kwanza ya kura isiyo rasmi ya kumtafuta mrithi wa António Guterres kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD, Rebeca Grynspan kutoka Costa Rica, ameibuka kinara katika duru ya kwanza ya kura isiyo rasmi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kumtafuta mrithi wa Katibu Mkuu wa sasa António Guterres. Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia, Grynspan alipata uungwaji mkono mkubwa zaidi kati ya wagombea saba walioshiriki kura hiyo ya siri.
Nafasi ya pili imechukuliwa na Balozi wa Guyana katika Umoja wa Mataifa Carolyn Rodrigues Birkett, huku Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi, akishika nafasi ya tatu. Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi Julai ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika Umoja wa Mataifa, Zénon Mukongo Ngay, amesema duru nyingine ya upigaji kura itatangazwa katika siku zijazo.
Matokeo ya kura hizo za majaribio hayatangazwi rasmi kwa umma. Katibu Mkuu wa sasa António Guterres anatarajiwa kumaliza muhula wake wa pili mwishoni mwa mwaka huu. Baraza la Usalama litampendekeza mshindi atakayepata angalau kura tisa kati ya wanachama 15 bila kuzuiwa na kura ya turufu ya mwanachama yeyote wa kudumu, kabla ya kuthibitishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.