Rais wa Marekani Donald Trump amemuarifu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu operesheni za Marekani katika eneo la Ghuba, ofisi ya Netanyahu imesema, baada ya Iran kuripoti mashambulizi mapya ya Marekani.
Afisa mmoja wa Marekani alithibitisha juu ya mazungumzo hayo ya simu siku ya Alhamisi, ingawa hakutoa maelezo zaidi.
Mvutano umeongezeka kati ya Trump na Netanyahu kuhusu namna ya kushughulikia vita dhidi ya Iran. Mzozo huo umemgharimu Trump kisiasa kutokana na kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa za matumizi wakati wa vita.
Gazeti la The Wall Street Journal aidha limeripoti jana, likinukuu vyanzo ambavyo havikutambulishwa kwamba Israel iliwaarifu Marekani kuwa vyombo vyake vya kijasusi viligundua njama mpya ya Iran ya kutaka kumuua Trump.
Iran imekuwa ikiahidi wazi kulipiza kisasi dhidi ya Trump tangu muhula wake wa kwanza wa urais, wakati Marekani ilipomuua Jenerali Qassem Suleimani wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).