Katika Mashariki ya Kati, mashambulizi ya anga yameanza tena Jumatano, Julai 29, baada ya utulivu wa siku kadhaa.
Jeshi la Marekani limetangaza kuwa limezuia makombora ya Iran, kisha likaanzisha shambulio la pamoja na Saudi Arabia dhidi ya wanamgambo wanaounga mkono Iran nchini Iraq, na kuwaua na kuwajeruhi watu wasiopungua kumi na wawili.
Angalau wanachama kumi wa muungano wa zamani wa wanamgambo wa Iraq wanaounga mkono Iran, ambao sasa wamejumuishwa katika jeshi, wameuawa katika mashambulizi ya anga kati ya Marekani na Saudi Arabia, vyanzo viwili ndani ya Kikosi cha Uhamasishaji cha Wananchi, Al-Hashd ash-Sha'bi, vimesema.
Saudi Arabia imethibitisha kuhusika katika mashambulizi hayo yaliyowalenga wanamgambo walio na mafungamano na Iran. Saudia imesema mashambulizi hayo ni jawabu la mashambulizi ya droni yaliyolenga miundo mbinu ya mafuta huko Sharqiya na Riyadh. Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia katika ujumbe iliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X imesema imefanya hivyo kutokana na "haki yake ya kujilinda."
Mashambulizi hayo yamelenga maeneo ya kikosi cha Al-Hashd ash-Sha'bi "katika majimbo kadhaa," lakini mashambulizi makubwa zaidi yameikumba eneo la Nineveh kaskazini mwa Iraq, na kuua watu 10, afisa mmoja amesema, akibainisha kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Haya yanafanyika baada ya Marekani kusema imetibua "shambulizi la kushtukiza" la Iran lililofanyika baada ya siku chache za utulivu baina ya nchi hizo mbili. Kulingana na Kamandi Kuu ya Marekani CENTCOM, imezuia mashambulizi ya makombora ya Iran Jumanne, ikidai makombora hayo yalikuwa yanavilenga vikosi vya Marekani huko Mashariki ya Kati.