Shirika la habari la Nation limetangaza kurejelea shughuli zake nchini Uganda, mwezi mmoja baada ya mkuu wa majeshi nchini humo, Muhoozi Kainerugaba, kuagiza lifungwe.
Mwenyekiti wa kampuni ya Taifa Group, ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu kutoka nchini Tanzania, Rostam Azizi, amesema kurejelewa kwa huduma za shirika hilo linalomiliki NTV Uganda, gazeti la Daily Monitor na redio kadhaa, kumefanikishwa na mazungumzo kati ya wadau wakuu, akiwemo Rais Yoweri Museveni na mkuu wa majeshi, ambaye pia ni mwanawe, Muhoozi Kainerugaba.
Haijabainika wazi ni nini kimechangia serikali ya Uganda kubadili msimamo wake wa kufungua tena vyombo vya habari mwezi mmoja baada ya wanajeshi, kwa agizo la Muhoozi, kuvamia makao makuu ya vituo hivyo na kuvifunga bila kutoa maelezo, huku wadau wakikosoa hatua ya serikali ya Uganda kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Mwaka 2013, serikali ya Uganda pia iliwahi kukifunga kituo cha NTV Uganda baada ya kupeperusha taarifa kuhusu nani atamrithi Rais Museveni. Wakati huu pia, Muhoozi Kainerugaba anahusishwa pakubwa na kumrithi babake.