Serikali Kuongeza Bajeti ya Elimu ili Kukidhi Mahitaji ya Mtaala Mpya

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuboresha bajeti ya elimu wakati ikitekeleza mtaala mpya wa elimu ili kuziba mianya ya mahitaji shuleni.

“Kwa kuwa tunaenda katika mtaala mpya wa elimu, tutaendelea kuboresha bajeti. Tutaendelea kuboresha bajeti kwa sababu mahitaji yanaongezeka kila wakati katika kumfanya mtoto asome vizuri,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, Alhamisi, Aprili 9, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Agnesta Lambert Kaiza, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua kauli ya Serikali juu ya kukomesha michango holela inayotozwa shuleni.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali haina shida na michango ya chakula ambayo imekuwa ikitolewa shuleni lakini akasisitiza kuwa endapo kutatokea michango mingine yoyote, ni lazima ifuate miongozo ya serikali na ipate baraka za Wakuu wa Mikoa husika.

Akitoa mfano wa michango ambayo haikubaliki, Waziri Mkuu amesema akiwa ziarani mkoani Katavi, alipokea malalamiko ya Mama mmoja ambaye mwanaye alizuiwa kujiunga na shule ya sekondari hadi atoe sh. 50,000/- ya dawati.

“Nilielekeza yule mtoto arudishwe shuleni na nimpongeze Mkuu wa Mkoa ambaye amenijulisha kuwa yule mtoto amesharudi shuleni. Lakini pia nilielekeza yule mwalimu mkuu naye aitwe na mamlaka za nidhamu, ahojiwe kwa uzembe wa kuona mtoto anakosa masomo kwa miezi miwili na wao wakaendelea na maisha kana kwamba hakuna jambo lililotokea,” amesema.

Mbali na changamoto hiyo, Waziri Mkuu amewapongeza walimu nchini kwa kujitoa bila kuchoka ili kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora. “Sote tunatambua kuwa walimu wengi wamejitoa sana katika baadhi ya maeneo. Licha ya wingi watoto na uchache wa walimu, kwa juhudi zao wamehakikisha wanakamilisha syllabus zao ili watoto wetu wapate elimu bora.”

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii