Shirika la upelelezi la Marekani, FBI, limemkamata mtu anayetuhumiwa kuvujisha taarifa za siri kuhusu kuangushwa kwa ndege ya kivita aina ya F-15E nchini Iran mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, mtuhumiwa huyo ni mfanyakazi wa zamani wa Kikosi Maalum cha Jeshi la Marekani (SOCOM), anayeshtakiwa kwa kusambaza taarifa za siri kwa chombo cha habari.
Tukio hilo lilizua taharuki kubwa, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akisema serikali yake ilikuwa ikifanya juhudi kubwa kumtafuta aliyekuwa akihusika na uvujishaji huo, akimtaja kama mtu “hatari” kwa usalama wa taifa.
Trump alionya kuwa taarifa hizo zilihatarisha maisha ya rubani aliyekuwa amepotea pamoja na operesheni ya uokoaji, kwani zilitoa mwanya kwa maadui kufahamu hali halisi ya tukio hilo.

Alieleza kuwa baada ya taarifa hizo kuvuja, mamlaka nchini Iran zilidaiwa kuweka zawadi kubwa kwa yeyote ambaye angefanikiwa kumpata rubani huyo aliyekuwa akiendelea kupambana kuokoa maisha yake.
Licha ya changamoto hizo, jeshi la Marekani lilifanikiwa kuwaokoa marubani wote wawili wa ndege hiyo, mmoja akitolewa muda mfupi baada ya tukio na mwingine kuokolewa baada ya operesheni ngumu iliyohusisha mamia ya wanajeshi na ndege za kijeshi, baadhi zikiwa chini ya mashambulizi.
Kwa upande wake, FBI imeonya kuwa itaendelea kuwachukulia hatua kali wote watakaohusika na uvujishaji wa taarifa za siri, ikisisitiza kuwa vitendo hivyo vinaweka maisha ya raia na wanajeshi hatarini.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime