Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, wilaya ya Geita, mkoani Geita, imemhukumu kifungo cha miezi sita jela Abdulazizi Kabangila, miaka 31 na mkazi wa Mwatulole baada ya kupatikana na hatia ya kutoa taarifa za uongo na kutekeleza shambulio la kudhuru mwili kwa Veradius Magogo asiyekuwa na hatia.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa, mnamo tarehe 06 Aprili 2026, majira ya saa 1:00 usiku katika eneo la starehe la The Vibes lililopo Manispaa ya Geita, Mshtakiwa alizua taharuki kwa madai kuwa amepoteza nguvu au maumbile yake ya siri baada ya kuguswa bega na mlalamikaji, Veradius Magogo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka na ushahidi uliotolewa, mshitakiwa akichochewa na imani potofu na nia ovu, alimvamia na kumshambulia Veradius Magogo na kumsababishia maumivu makali mwilini huku akihamasisha kundi la watu kutaka kujichukulia sheria mkononi.
Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na Madaktari kutoka Hospitali ya Serikali ulithibitisha pasi na shaka kuwa madai ya mshitakiwa yalikuwa ni ya uongo na upotoshaji, kwani viungo vyake vilikutwa vikiwa katika hali ya kawaida ya kimaumbile.
Mnamo tarehe 08 Aprili 2026, katika shauri la jinai namba CC 308/2026, mbele ya Hakimu Mfawidhi Mheshimiwa Ally Mgomba, Mahakama ilijiridhisha na ushahidi wa upande wa Jamhuri.
Aidha mahakama imemtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la Shambulio la Kudhuru Mwili kinyume na Kifungu cha 241 cha Sura ya 16 ya Kanuni ya Adhabu (kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023). Kutokana na uzito wa kosa hilo na athari za kijamii zinazotokana na uzushi wa aina hiyo, mshitakiwa amehukumiwa kwenda jela miezi sita (6) bila faini.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime