Trump Aibua Taharuki, Akutana na Katibu Mkuu wa NATO, Atishia Kujiondoa

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameibua mjadala mkubwa wa kimataifa baada ya kutoa kauli kali dhidi ya muungano wa kijeshi wa NATO, kufuatia mkutano wake wa faragha na Katibu Mkuu wa muungano huo, Mark Rutte.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu ya White House, ilitarajiwa kuwa viongozi hao wangejadili namna ya kupunguza mvutano uliotokana na vita kati ya Iran na Marekani. Hata hivyo, baada ya mkutano huo, Trump alionekana bado kutoridhishwa na mchango wa NATO katika mgogoro huo.

Kupitia ujumbe aliouandika kwa herufi kubwa kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema, “NATO haikuwa nasi tulipowahitaji, na haitakuwa nasi tukiwahitaji tena.” Kauli hiyo imezua hofu kuhusu mustakabali wa ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya.

Kauli ya Trump inakuja wakati dunia ikishuhudia athari za kufungwa kwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya Strait of Hormuz, jambo lililochangia kupanda kwa bei za nishati duniani. Licha ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda kati ya Marekani na Iran, mvutano bado unaonekana kuathiri mahusiano ya kimataifa.

Aidha, Trump amekuwa mkosoaji wa muda mrefu wa NATO, akisisitiza kuwa baadhi ya nchi wanachama hazichangii vya kutosha katika bajeti ya ulinzi. Pia aliwahi kuibua hoja ya kutaka Marekani kudhibiti eneo la Greenland, hatua iliyopingwa na baadhi ya washirika wake, hususan Denmark.

Kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa mwaka 2023, Rais wa Marekani hawezi kujiondoa NATO bila idhini ya Bunge, jambo linaloweza kuwa kikwazo kwa azma hiyo endapo Trump ataamua kuitekeleza.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii