Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Machi 30, 2026 amepokea ripoti mbalimbali kutoka taasisi za umma katika Ikulu ya Dar es Salaam.
Ripoti hizo ni pamoja na za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), TAKUKURU, na PPRA, zikiwasilishwa na viongozi wa taasisi hizo mbele ya Rais.
Katika taarifa ya TAKUKURU iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu Crispin Francis Chalamila, imebainika kuwa uchunguzi wa mwaka 2024/2025 umefichua wizi wa shilingi bilioni 147.5 kupitia kughushi kadi za benki, ambapo fedha hizo zilichotwa kutoka akaunti za wateja bila idhini yao.
Ameeleza kuwa fedha hizo zilitumika kupitia kadi 1,551 za wateja kutoka mataifa 11, zikihusisha makampuni 162 na benki tano za ndani. Aidha, kadi hizo zilitumika kulipia huduma mbalimbali ikiwemo utalii, usafirishaji, kodi na bima ya afya, huku baadhi ya watuhumiwa wakijihusisha na utakatishaji fedha uliosababisha hasara ya shilingi bilioni 2.6 kwa baadhi ya benki.

Hata hivyo TAKUKURU imefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 14.5 kupitia oparesheni zake, ambapo kati ya hizo, bilioni 10.1 ni fedha taslimu zilizorejeshwa serikalini na bilioni 4.4 ni mali na vifaa vilivyookolewa kutoka miradi ya maendeleo.
Kwa upande wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ripoti iliyowasilishwa na Charles Kichere imeeleza kuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) limepata hasara ya shilingi bilioni 3.06 kutokana na ajali 328 za treni, zilizosababisha uharibifu wa miundombinu na kupungua kwa mapato.
Dkt. Kichere amesema changamoto hizo zinatokana na udhaifu katika usimamizi na matengenezo ya miundombinu, hasa katika reli ya zamani (MGR), huku akipendekeza kuimarishwa kwa ukaguzi wa mara kwa mara pamoja na kuanzishwa kwa mfumo madhubuti wa bima kwa mali za shirika hilo.
Aidha, CAG amesema hakuweza kukikagua CHADEMA kutokana na mashauri yanayoendelea mahakamani, huku vyama vya CUF na NRA vikipewa hati zenye mashaka kutokana na kasoro za kifedha, ikiwemo upungufu wa nyaraka na matumizi yasiyothibitishwa.
Hata hivyo matukio hayo yameambatana na picha mbalimbali zikimuonesha Rais Samia akipokea na kukabidhiwa ripoti hizo, zikiakisi uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime