Vita dhidi ya Iran vyavuuka mwezi mzima

Vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran vimeingia siku yake ya 31, huku kila upande ukizidisha mashambulizi na vitisho dhidi ya mwengine na vikigeuka kuwa vya kikanda.

Jeshi la Israel lilisema liliyadunguwa makombora mawili yaliyovurumishwa kutokea nchini Yemen mapema asubuhi ya Jumatatu (Machi 30) yakiwa mashambulizi ya pili kutokea Yemen, baada ya yale ya Jumapili asubuhi, ambapo wapiganaji wa Kihouthi walitangaza rasmi kujiunga na vita hivyo upande wa Iran.

Miripuko mikubwa pia ilisikika usiku wa kuamkia Jumatatu katika maeneo mbalimbali nchini Israel, likiwemo eneo la viwanda la Beersheba.

Nchini Iran kwenyewe, vyombo vya habari vya huko viliripoti kuwa mojawapo ya mitambo kwenye eneo la viwanda vya kemikali za petroli mjini Tabriz umeshambuliwa lakini hakukuwa na taarifa za kuvuja kwenye kemikali za hatari.

Jeshi la Israel lilisema kuwa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita ndege zake za kivita zilikuwa zimedondosha zaidi ya mabomu 120 mjini Tehran yaliyolenga maeneo yanayohusika na utafiti na utengenezaji wa silaha.

Miongoni mwa majengo yaliyoshambuliwa ni vyuo vikuu, jambo ambalo lililifanya jeshi la Iran kuonya kwamba sasa  lingevilenga vyuo vikuu  vya Israel na vile vyenye mahusiano na Marekani kwenye eneo zima la Mashariki ya Kati, pamoja na makaazi binafsi ya maafisa na wanasiasa wa Israel na Marekani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii