Trump adai mabadiliko ya utawala yamefanikiwa Iran
Rais Donald Trump wa Marekani amedai kwamba vita vilivyoanzishwa na nchi yake na Israel vimeshafanikiwa kuleta mabadiliko ya utawala nchini Iran, huku akihakikisha kuwa ataweza kufikia makubaliano na Wairani.
Akizungumza na waandishi mjini Washington siku ya Jumatatu (Machi 30), Trump aliyataja majina ya viongozi kadhaa wa Iran waliokwishawauwa kwenye vita hivyo ambavyo vimetimia mwezi mzima sasa.
Rais huyo wa Marekani alisema kwa sasa wanashughulika na viongozi tafauti kabisa, jambo ambalo linamfanya aone kuwa "tayari kuna mabadiliko ya utawala."
Kauli hiyo ya Trump ilitolewa wakati mawaziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Saudi Arabia na Misri wakirejea nyumbani baada ya mkutano wao nchini Pakistan uliojadili hatua zilizopigwa katika juhudi za kuzileta Iran na Marekani kwenye meza ya mazungumzo kukomesha vita hivyo.
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Pakistan haikutowa undani wa majadiliano hayo, lakini Spika wa Bunge wa Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba vikosi vya nchi yake vinangojea kuwakabili wanajeshi wa Marekani kuwasili nchini humo wakati wowote.
Tayari kikosi cha wanajeshi wa Marekani 2,500 wa ziada kimewasili kwenye eneo la Mashariki ya Kati, ikikhofiwa kuwa ni kwa ajili ya kuivamia Iran kupitia ardhini.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii