Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa Makamu wake, J.D. Vance, sasa atasimamia mapambano dhidi ya udanganyifu nchini humo, akimtaja rasmi kama “Fraud Czar”.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye Truth Social, Trump alisema kuwa tatizo la udanganyifu nchini Marekani ni kubwa na limeenea, hivyo jukumu la Vance litakuwa muhimu katika kuhakikisha fedha za walipa kodi zinalindwa.
“Tutamwita ‘Fraud Czar’, na atahusika kila mahali, hasa katika majimbo ambayo yamekuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma,” alisema Trump, ingawa hakutoa ushahidi wa moja kwa moja kuunga mkono madai hayo.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani, hatua hiyo inatokana na amri ya kiutendaji iliyosainiwa Machi 16, inayolenga kuanzisha kikosi kazi maalum cha kitaifa kupambana na udanganyifu, ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali katika programu za serikali.
Chini ya mpango huo, Vance ndiye mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, ambacho kinatarajiwa kuratibu mikakati ya kitaifa ya kupambana na udanganyifu katika ngazi zote za serikali.
Akizungumza kabla ya kikao cha kwanza cha kikosi hicho, Vance alisema mapambano dhidi ya udanganyifu yanahitaji ushirikiano wa serikali nzima.“Hii siyo tu wizi wa fedha za wananchi, bali pia ni wizi wa huduma muhimu wanazotegemea,” alisema.
Katika kipindi cha hivi karibuni, utawala wa Trump umeelekeza nguvu zaidi katika kushughulikia madai ya udanganyifu, hasa katika majimbo kama California na Minnesota, hatua ambayo imeibua mjadala wa kisiasa.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa majimbo hayo wamepinga madai hayo, wakisema tayari wamekuwa wakichukua hatua za kukabiliana na udanganyifu kwa muda mrefu.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime