POLISI MWANZA WAFANYA OPARESHENI KALI, WAKAMATA VYOMBO 120 NA MADEREVA WANAOKIUKA SHERIA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetangaza kuendesha oparesheni maalum ya kudhibiti ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, ikilenga hasa madereva wa pikipiki na bajaji wanaochangia ongezeko la ajali na kero kwa watumiaji wengine wa barabara.

Oparesheni hiyo iliyoanza Machi 31, 2026 inaendelea hadi sasa, ikijikita katika kukomesha vitendo vya kufunga taa kali zisizoruhusiwa, kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, kutovaa kofia ngumu (helmet), kutumia namba za usajili zisizo halali, kubeba abiria kupita kiasi pamoja na kuendesha bila leseni.

Katika utekelezaji wake, jumla ya vyombo 120 vimekamatwa, vikiwemo pikipiki za magurudumu matatu 98, pikipiki za kawaida 5 zilizobainika kukatwa ‘mafla’ na kupiga kelele, magari ya abiria 13 pamoja na magari madogo 4.

Aidha, madereva saba walikamatwa kwa kosa la kuendesha wakiwa wamelewa pombe.

Polisi pia wamewafungia leseni madereva sita waliobainika kuendesha wakiwa wamelewa, huku wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Madereva hao walikamatwa Aprili 3, 2026 na kufungiwa leseni zao kwa muda wa miezi sita kuanzia Aprili 4, 2026.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, likisisitiza kuondoa taa zisizoruhusiwa, kutumia namba halali za usajili na kuhakikisha wanakuwa na leseni stahiki.

Aidha wananchi wote wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinda usalama barabarani kwa kufuata sheria wakikumbushwa kuwa usalama wa barabarani ni jukumu la kila mmoja.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii