Waomba huduma ya kipolisi irejee, RPC Mutafungwa awataka kutunza amani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ameridhia ombi la wananchi wa Kata za Mabatini na Mbugani, Wilaya ya Nyamagana, la kurejesha huduma za kipolisi katika Kituo cha Polisi Mabatini kilichoharibiwa wakati wa vurugu za Oktoba 2025.

Hayo yamejiri wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika march 22, 2026 katika uwanja wa Shule ya Msingi Mabatini "B", uliowakutanisha wananchi wa kata hizo mbili na Jeshi la Polisi.

​Akizungumza na wananchi kupitia mkutano huo, Kamanda alisema amesikia kilio chao cha muda mrefu na akawahakikishia kurejesha huduma hiyo, kwa kuwa wananchi wenyewe wameamua kukikarabati kituo hicho kilichoharibiwa na kuchomwa moto.

Aidha, Kamanda alisema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa jukumu la kuzuia uhalifu si la Jeshi la Polisi pekee, wala si la viongozi wa Serikali za Mitaa peke yao, bali ni jukumu la wananchi wote kwa sababu wahalifu wanatoka miongoni mwa jamii.

Alisisitiza kuwa watawadhibiti wahalifu kwa kukataa uhalifu, na ni lazima wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza waelewe dhana hiyo.

​Pia, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuviunga mkono vikundi vya vijana vitakavyoanzishwa na wakaguzi wa kata vitakavyoshiriki katika michezo mbalimbali, kwani Jeshi la Polisi lina utaratibu wa kuzuia uhalifu kupitia michezo (Youth and Sports).

​Vilevile, Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi limeamua kutoka maofisini baada ya hali ya mkoa kuwa shwari; sasa wanaenda kuwafuata wananchi waliko ili wasaidiane nao kuzuia na kudhibiti uhalifu.

​"Tunataka siku moja wananchi wafike vituo vya Polisi kusalimia tu, lakini siyo kwa ajili ya changamoto za kiusalama," alieleza Kamanda Mutafungwa.

​Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa mitaa sita ya kata hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mabatini, Paulo Mpozemenya, alisema wamefanya jitihada za kukarabati kituo hicho na wameomba Kamanda aridhie kukifungua ili huduma zirejee kama awali, kwani matukio ya uhalifu yameanza kuongezeka.

​Kwa upande wake, Mkaguzi wa Kata hiyo, Mkaguzi (Insp.) Shaban Kashakala, alisema Kata ya Mabatini ina jumla ya vikundi sita vya ulinzi vilivyo chini ya viongozi wa mitaa husika, na kazi yake imekuwa ni kutoa elimu ya namna ya ulinzi shirikishi na ukamataji salama.

​Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana (OCD), SSP Virginia Sodoka, amewashukuru wananchi wa Kata za Mabatini na Mbugani kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia na kudhibiti uhalifu.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii