Serikali yashtakiwa kwa kuendelea kuzingira makazi ya Bobi Wine

Chama cha wanasheria nchini Uganda, ULS, kimeishtaki serikali ya Uganda kwa kile chama hicho kimesema polisi kuendelea kuzingira makazi ya mwanasiasa wa upinzani, Robert Kyagulani, maarufu kama Bob Wine.

Katika kesi waliyofungua Machi 16, wanasheria wa chama hicho wanavituhumu vikosi vya usalama kuendelea kusigina katiba na sheria za nchi kwa kuzingira makazi ya Bob Wine, tangu kumalizika kwa uchaguzi wa mwezi Januari mwaka huu.

Akihojiwa na kamati ya bunge kuhusu usalama wiki iliyopita, mkuu wa jeshi la Polisi alitetea uwepo wa askari wake kwenye makazi ya Bob Wine, akisema watabakia hapo hadi pale watakapojiridhisha kuwa makazi ya mwanasiasa huyo yako salama.

Tangu kufanikiwa kuwatoroka polisi baada ya uchaguzi wa Januari 15, polisi wamekuwa wakikataza ndugu, marafiki, viongozi wa chama na hata mawakili kuingia ndani ya nyumba yake, hata kwa kupeleka chakula.

Haya yanaendelea wakati Robert Kyagulani mwenyewe akiwa ametangaza kuikimbia nchi yake kwa kuhofia usalama wake, ambapo wiki iliyopita alifanya ziara Marekani na Ulaya kukutana na wadau wa demokrasia, kuwashawishi kuweka shinikizo kwa serikali ya Uganda.

Jeshi la Uganda na polisi wamekuwa wakimsaka Kyagulani kwa tuhuma za uchochezi madai ambayo chama chake cha NUP kimeyatupilia mbali, kikisema msako huo umeagizwa na mtoto wa rais Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii