Jeshi la polisi mkoa Mwanza tangu tarehe 20/03/2026 usiku liliwakamata na linaendelea kuwahoji watu watatu (3) ambao ni askari mgambo kwa tuhuma za mauaji ya kijana aitwaye Rashid Masunga Nyandonga, miaka 31, kazi yake ni fundi simu na mkazi wa Bugando jeshini wilaya ya Nyamagana.
Watuhumiwa hao waliokamatwa majina yao ni:-1. Zongoli Richard Makongoro, miaka 38, kazi yake ni askari mgambo anayefanya kazi katika kata ya Mahina na mkazi wa Bugarika wilaya ya Nyamagana.
2. Genge Chacha Mwita, miaka 45, kazi yake ni mgambo anayefaya kazi katika kata ya Igogo na mkazi wa mtaa wa Kambarage wilaya ya Nyamagana.
3. Ibrahim Chacha Mwita, miaka 25, kazi yake ni askari mgambo katika kata ya Pamba na mkazi wa Bugando mission, wilaya yaNyamagana.
Tukio hili la mauaji lilitokea tarehe 20/03/2026 majira ya 12:45 jioni huko mtaa wa Mission katika eneo la Sahara, kata ya Pamba, wilaya ya Nyamagana.
Inadaiwa kuwa jioni hiyo ya tukio hilo askari mgambo hao wakiwa katika mtaa huo walimtilia shaka marehemu Rashid Masunga Nyandonga kuwa anauza dawa za kulevya aina ya Mirungi na kuanza kumfuatilia, ndipo mtu huyo alikimbia mbio kukwepa kukamatwa.
Askari hao mgambo walimfukuza na kufanikiwa kumkamata akiwa na mirungi gramu 50 ingawa mtu huyo alikuwa akihema kwa nguvu na kuonyesha dalili za kuishiwa nguvu.
Askari hao wa mgambo walimpeleka katika hospitali ya Sekou Toure kwa huduma zaidi na wakati matibabu yakiendelea hospitalini hapo alifariki dunia.
Kutokana na hali hiyo jeshi la polisi mara moja liliwakamata askari mgambo hao wote watatu kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Askari mgambo hao wakati wakifanya ukamataji kwa mtuhumiwa huyo kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya walikuwa peke yao na wakati huo jeshi la polisi mkoa wa Mwanza halikuwa na operesheni yoyote ya ukamataji wa makosa iliyowashirikisha askari mgambo katika eneo hilo.
Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi (post mortem) tarehe 21/03/2026 katika hospitali ya Sekou Toure ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Ndugu wa marehemu wameshiriki katika uchunguzi huo kwa mujibu wa taratibu na umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya utaratibu wa mazishi.
Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza kuhusiana na tukio hili linaendelea na uchunguzi wa kina na endapo ushahidi utaonesha kuwa watuhumiwa hawa wamehusika na mauaji hayo watawajibishwa kwa mujibu wa sharia.
Pia tunaomba askari mgambo wanapofanya ukamataji wazingatie ukamataji salama na wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kufichua uhalifu na wahalifu.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime