Wafanyabiashara wakoshwa mapendekezo tume ya Rais ya kodi

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe, amesema wamefurahishwa na ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mifumo ya Kodi nchini, kwa namna ilivyoakisi maoni na mapendekezo yao.

Amesema ingawa baadhi yao walikuwa na mashaka na uundwaji wa tume hiyo kwa kuwa ilihusisha maofisa wa Serikali na haikuwa na wajumbe kutoka kundi la wafanyabiashara, lakini ripoti yake imekata kiu na kugusa yale yanayolalamikiwa.

Hata hivyo, mashaka dhidi ya tume zinazoundwa na Rais kushughulikia masuala mbalimbali nchini, yameshuhudiwa mara kadhaa. Ingawa mara nyingi tume hizo huja na ripoti zinazokidhi matarajio ya umma.

Livembe, ameeleza hayo Alhamisi Machi 19, 2026 alipozungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, baada ya tume hiyo iliyoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue kukabidhi ripoti yake kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Machi 18, mwaka huu.

“Hoja zetu zimesikilizwa na zimeonekana za msingi, kwa sasa tunavuta subira kuona mambo yanakwenda vizuri sana kwa tulivyosikiliza mapendekezo ya tume na mapokeo ya Rais,” amesema.

Livembe, amesema baadhi ya wafanyabiashara walikuwa na mashaka na tume hiyo kwa kuwa haikuwa na wafanyabiashara ndani yake, lakini ripoti yake imefuta malalamiko yote kwani imejibu kilio chao.

“Ilikuwa na maofisa wa Serikali watupu kwa hiyo ilipoteza imani kwamba haitafanya kazi kama ilivyokusudiwa, lakini kwa hoja zilizotolewa tunakubaliana kwamba tume ni sahihi na inaaminika,” amesema.

Hata hivyo ameipongeza tume kwa kuwa na usikivu na kuja na mapendekezo yaliyogusa hoja zote zilizokuwa zinalalamikiwa na wafanyabiashara.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii