Idadi ya watu waliouawa katika mashambulio Iran yapita 3100

Zaidi ya watu 3,186 wameuawa nchini Iran tangu kuzuka kwa mapigano Februari 28 kulingana na Shirika la kutetea haki za binadamu (Hrana) lenye makao yake nchini Marekani.

Kati ya watu hao waliouawa,1,394 walikuwa ni raia wakiwemo karibia watoto 210 limesema shirika hilo.

Aidha lishirika hilo limeeleza kwamba wanajeshi 1,153 wa Iran wameuawa kwenye mapigano hayo wakati 639 wakikosa kutambulika.

Israel na Marekani zimekuwa zikiishambulia Iran kwa makombora, Iran nayo ikijibu mashambulio hayo kwa kulenga kambi za kijeshi za Marekani na miundombinu yake mashariki ya kati.

Tehran pia imerusha makombora nchini Israel. Mapigano yakiendelea wakati huu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizitaka Iran, Marekani na Israeli kusitisha mapigano na kufanya mazungumzo.

Katika hatua nyengine, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth , amesema hakuna muda uliowekwa kwa vita vinavyoendelea nchini Iran kufika mwisho.

Hii imekuwa wiki ya tatu tangu Marekani na Israeli, walipoanza mashambulizi jijini Tehran kwa lengo la kuhakikisha kuwa nchi hiyo haitengenezi silaha za nyuklia.

Aidha, Wizara ya Ulinzi nchini Marekani imepanga kuomba kuidhinishwa kwa Dola nyingine Bilioni 200 kutoka kwenye bunge la Congress, ili kuendelea na vita hivyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii