Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah akiwa katika Iftari iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar Machi 17, 2026 amesema Serikali haitawavumilia wale wote wanaokwepa Kodi kwa kujihusisha na biashara za Magendo.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi kwenye Iftari hiyo iliyohudhuriwa na Walipakodi Visiwani Zanzibar pamoja na watumishi wa TRA katika hoteli ya Madinat Al Bahr Makamu wa Pili wa Rais SMZ Hemed amesema vyombo vya dola vipo imara kufuatilia wanaokwepa kodi na kuchukua hatua.
Amesema Serikali ipo bega kwa bega na TRA kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kukusanya kodi na kuwasaidia kupambana na wote wanaokwepa kodi maana wamekuwa wakiidhoofisha nchi kwa kuikosesha mapato.
“Hakuna unafiki kwenye masuala ya kodi, Kama unawapenda viongozi wetu wakuu lipa kodi kwa uaminifu ili kuwawezesha kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwahudumia wananchi” amesema Makamu wa Pili wa Rais SMZ.