Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, amewakumbusha Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali mkoani humo, kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja na siyo bora huduma.
Agizo hilo limetolewa wakati wa Baraza la Kamanda wa Polisi Mkoa lililowakutanisha Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCDs), Wakuu wa Vikosi, Waratibu Polisi jamii wilaya, Wakaguzi wa Kata, pamoja na askari wa vyeo mbalimbali kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi na nidhamu.
Akizungumza katika baraza hilo, DCP Mutafungwa amesisitiza kuwa mteja wa ndani na nje wa Jeshi la Polisi anapaswa kuhudumiwa kwa weledi na heshima, jambo ambalo ni nguzo muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Polisi na jamii.
"Ni lazima tujikite katika kutoa huduma bora na siyo 'bora huduma'. Katika usimamizi wa sheria, hususan usalama barabarani, tujikite zaidi kutoa elimu na maonyo kwa makosa yanayorekebishika kuliko kukimbilia kuchukua hatua za kisheria kila wakati. Kauli njema kwa mteja ndiyo siri ya mafanikio yetu," amesema Kamanda Mutafungwa.
Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoani humo SSP Sunday Ibrahim, ameahidi kusimamia nidhamu kwa askari na kuzuia makosa ya usalama barabarani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kwimba, Mrakibu wa Polisi (SP) Mkandala, amewahimiza askari na wakaguzi kutojitenga na jamii, bali washiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii, ikiwemo nyakati za furaha na shida, ili kujenga imani na ukaribu na wananchi wanaowahudumia.
Naye mkaguzi wa Kata ya Mabatini, Mkaguzi wa Polisi (INSP) Shaban Kashakara, akizungumza kwa niaba ya Wakaguzi wa Kata, amemhakikishia Kamanda Mutafungwa kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kikamilifu katika ngazi za mitaa ili kuhakikisha jamii inabaki kuwa salama na yenye amani.
Wakuu wa Polisi wa Wilaya waliohudhuria baraza hilo wamekiri kupokea maelekezo na kuahidi kuimarisha usimamizi wa karibu kwa askari walio chini yao. Lengo kuu ni kuhakikisha kila askari anatekeleza majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu, hatua itakayosaidia kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa Jeshi la Polisi Mkoani humo.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime