Kisa Mabala kuukana uraia wa Uingereza

Ukikutana naye kwa mara ya kwanza, hutaamini kuwa mzungu huyu ni raia wa Tanzania na tena ni mlumbi wa Kiswahili pengine kuliko Waswahili wengi wa asili.

Wengi waliosoma vitabu vyake wakiwa shule za sekondari vya ‘Mabala the Farmer na ‘Hawa the Bus Driver’, wanakumbuka jinsi alivyoeleza mazingira ya Tanzania na maisha wanayopitia.

Huyo ndiye Richard Mabala, ambaye kwa sasa amefikisha miaka 49 ya kuishi Tanzania tangu alipokuja nchini akitokea Uingereza mwaka 1973.

Alikuja na wenzake kwa ajili ya kutekeleza program ya kujitolea, akiwa mwalimu wa lugha ya Kifaransa na alipangiwa kuishi nchini miaka miwili tu, lakini akajikuta akilowea na kusahau kabisa alikotoka.

Siyo tu alijifunza lugha ya Kiswahili na baadaye kuja kuwa mlumbi (mahiri katika matumizi), bali aliamua kubadilisha jina lake la awali la Richard Frank Satterthwaite na kujiita jina alilopewa na Wanyamwezi la Mabala analotambulikana nalo hadi leo.

Baada ya kuishi miaka tisa nchini, akiwa na wito zaidi wa kufundisha watoto wa Kitanzania, mwaka 1982 aliamua kuomba uraia na hatimaye kupewa na sasa anaadhimisha miaka 40 ya uraia huo.

Hakutaka kurudi tena kwao Uingereza, kwani tangu akiwa huko kabla ya kuja nchini, alikuwa akivutiwa na mitazamo ya Mwalimu Julius Nyerere kupitia kauli na maandishi yake, hivyo fursa ya kuja Tanzania na kuyaishi yale aliyokuwa akiyasoma, ikamtamanisha kuongeza muda wa kuishi nchini.

“Kabla sijajua kama ningekuja Tanzania, nilikuwa nasoma hotuba za Nyerere. Ilipotokea nafasi ya kuja ikawa fursa kwangu kuyaona yale niliyokuwa nayasoma na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Nilipanga kukaa miaka miwili, hata hivyo ilipoisha sikuondoka,” anasema Mabala ambaye alichoshwa na ubepari sambamba na sera za nchi yake,

Anaongeza: “Nilianza kuongeza mwaka mmoja mmoja, hatimaye ikafika muda ikabidi nitafakari na kufanya uamuzi nichague kuomba uraia au niondoke kurejea Uingereza, nikaona bora kuomba uraia; ni uamuzi sahihi na tangu hapo maisha yangu yakawa Tanzania.’’

Anasema ndugu na wazazi hawakuwa na pingamizi, walikubaliana na uamuzi wake na hata kumwita kwa jina lake jipya la Richard Mabala.

Alipoingia nchini alipangiwa kufundisha somo la Kifaransa kabla ya kubadili na kuwa mwalimu wa Kiingereza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Milambo ya mkoani Tabora. Hapo ndipo alipokutana na wanafunzi wake ambao baadhi wamewahi kushika nafasi kubwa katika uongozi hasa wa kisiasa. Viongozi hao ni pamoja na aliyewahi kuwa mbunge na waziri, Dk Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi.

Wengine ni marehemu Profesa Jwani Mwakyusa, aliyekuwa msomi mbobezi wa sheria, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, Othman Rashid, Mkurugenzi Mstaafu wa Usalama wa Taifa na wengineo wengi.

Kabla ya kujiunga na kwaya, jina lake lilikuwa linasomeka kama Richard Frank Satterthwaite, lakini kutokana na waimbaji wenzake na watu waliokuwa wakimzunguka kanisani kushindwa kulitamka jina lake la pili, wakaamua kumuita Mabala.

“Baada ya kunizoea kwenye kwaya wenzangu wakaniambia jina langu ni gumu kutamka, hivyo wataniita Mabala. Nakumbuka hiyo ilikuwa mwaka 1974 na hata nilipowaalika wazazi wangu kuja nchini kabla sijaamua kuchukua uraia walilikuta jina hilo.

Kwa kuwa niliona hilo limefanyika kwa upendo sikuwa na sababu ya kukataa, kuanzia hapo nikawa naitwa Richard Mabala na hata nilipoomba uraia nilipeleka jina hilo na ilipofika 1982, nilipewa uraia na hati yangu ya kusafiria ikawa inasomeka rasmi kama Richard Mabala,” anasema Mabala, ambaye mbali ya Mirambo amefundisha pia sekondari za Mzumbe, Kibosho na vyuo vya ualimu kama Chang’ombe na Marangu.

Mabala, aliyeteka hisia za wengi kwa vitabu vyake vya kitaaluma shuleni, amekuwa mwanaharakati aliyejikita katika masuala ya elimu, jinsia na maendeleo ya vijana.

Ni mmoja wa waanzilishi wa azaki, zikiwamo za shirika la Hakielimu na Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP). Nje ya uandishi wa riwaya, ameandika machapisho mengi kuhusu stadi za maisha, jinsia na vijana.

Akizungumzia elimu ya Tanzania, anasema dosari mojawapo kubwa ni Tanzania kuendelea kukumbatia Kiingereza kama lugha ya kufundishia.

Anasema Kiingereza kinaweza kufanya vizuri zaidi kwa mazingira ya Kitanzania kama kitafundishwa kama lugha ya pili au ya tatu, lakini sio kuwa lugha ya kufundishia kwa sababu kimekuwa kikwazo cha wanafunzi kukosa ujuzi na kuishia kukariri.

Huwezi kuamini kuwa mtu mgeni aliyekuja nchini akiwa mtu mzima, angeweza kuandika vitabu vilivyosadifu maudhui na mazingira ya Kitanzania.

Hilo halikuwa tatizo kwa Mabala, ambaye mbali ya utunzi wa vitabu vya kitaaluma, amebobea pia katika dunia ya uandishi wa makala za uchambuzi.

Huko anapenda kujulikana kwa jina la ‘Makengeza’ analotumia kuandika katika gazeti la Mwananchi na Aya za Bint Hidaya katika gazeti la Raia Mwema.

Kinachompambanua katika uandishi wa makala zake, ni namna anavyofikisha ujumbe kwa kutumia mitindo ya kilugha kama lugha ya picha, ucheshi, kejeli na hata mafumbo.

Kwa nini aliviandika vitabu hivi vilivyotokea kuwa na mvuto kwa wanafunzi wengi? Anaeleza: “Sikutegemea kama vitabu hivi vingekuwa vinasomwa hadi leo, nashukuru kwa Watanzania kuvielewa na kuvikubali vitabu hivi, kiukweli najivunia. Niliviandika kwa hasira, hakukuwa na vitabu vidogo kwa ajili ya kusoma watoto wa kidato cha kwanza na pili vyenye asili ya Afrika.

“Waingereza walikuwa wanaleta vitabu vyao ambavyo havina uhalisia kabisa na maisha ya Mwafrika, ndipo nikaandika Mabala the Farmer, walipokubali nikaandika Hawa the Bus Driver. Vyote hivi vinagusa mazingira ya Kiafrika, tena nililenga zaidi Kitanzania.

Mwalimu mstaafu Bakari Heri, leo anajivunia uwezo kiasi alionao katika lugha ya Kiingereza, lugha anayosema aliisomea alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Mimi ni mwalimu na fani yangu ni ualimu wa Kiingereza na Literature. Nimesoma vitabu vingi nikiwa sekondari, lakini nikiri Mabala the Farmer nacho kilikuwa katika orodha. Inawezekana nacho kilinijenga katika maarifa niliyonayo. Enzi hizo sikujua kama mtunzi wake ni mtu wa nje tena mzungu. Niseme Mr Mabala ameacha legacy (urithi) katika elimu,’’ anasema mwalimu Heri.

Kutoka Mabala the Farmer anasema baadaye alitunga kitabu alichokiita ‘Mabala and the Internet’, kitabu kinacholenga kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya mitandao.

“Mabala huyu ni yule yule ila sasa kijana wake amemaliza chuo kikuu na amebobea kwenye masuala ya Tehama, lakini baba anajaribu kuonyesha kuwa anafahamu vyema teknolojia kuliko kijana wake. Katika kipindi hiki ambacho matumizi ya intaneti yameshika kasi, nimeandika kuelimisha jamii ijue matumizi sahihi ya intaneti na mitandao ya kijamii,’’ anaeleza Mabala, ambaye pia ni mtunzi mahiri wa mashairi, yakiwamo yaliyowahi kuchapishwa katika kitabu cha Summons- Poems from Tanzania.

Mabala sio tu aliukana uraia wa Uingereza, anaonekana zaidi kuvutiwa na desturi za Kitanzania.

Hili linadhihirishwa na mapenzi yake kwa lugha ya Kiswahili ambayo pengine anaweza kuwazidi Waswahili wenyewe.

Leo Mabala amekuwa sio mtetezi wa kutaka Kiswahili kitumike kufundishia shuleni, lakini pia ni mlumbi na bingwa wa lugha hiyo. Licha ya kutokuwa na asili ya Tanzania, Mabala ni Mswahili kuliko Waswahili kwa namna ya anavyoijua sarufi na msamiati wa Kiswahili.

Anasema akiwa Mirambo alikuwa mshiriki mzuri wa shughuli za kanisani, ikiwamo kuimba kwaya, jambo analosema lilimjengea msingi mzuri wa kukijua Kiswahili.

“Kupitia ile kwaya nilijifunza zaidi Kiswahili na ilinisaidia kwa kiasi kikubwa kufahamu maneno ya lugha hiyo na mazingira sahihi yanapotumika, baada ya mwaka nilikuwa tayari nazungumza vizuri,” anasema.

Mapenzi yake kwa Kiswahili ndiyo yanayomsukuma kutaka lugha hiyo itumike kufundishia shuleni, akisema ni muhali kwa watoto wa Kitanzania wanaoishi mazingira ya Kiswahili, wakafundishwa kwa lugha ya kigeni na mwishowe wakawa na mafanikio ya kielimu. Anasema athari ya kufundisha kwa Kiingereza ni kuwakosesha watoto ujuzi, huku wakibaki kukariri yanayofundishwa.

“Binafsi siifahamu nchi yoyote ambayo lengo la elimu ni kujua lugha, ninavyofahamu lengo la elimu ni kujifunza na kupata ujuzi. Ni vigumu kupata ujuzi kama huelewi kinachofundishwa, hivyo utaishia kukariri ili uweze kujibu mtihani, sasa kwa mtindo huo ni vigumu kupata ujuzi.

“Mtu akiyapata yale maarifa au ujuzi anaofundishwa atautumia kuchambua mambo, hiyo itamwezesha kutoka hatua moja kwenda nyingine, lakini hiki kilichopo sasa ni mwanafunzi kulazimika kukariri Kiingereza cha kujibia maswali,” anasema Mabala.

Anasema mwaka 1982 taasisi moja ya Uingereza ilifanya utafiti nchini na kubaini kuwa ni robo tu ya wanafunzi wa sekondari ndio wanaokimudu Kiingereza cha kuweza kujifunzia masomo yote. Lakini wengi wanabahatisha au kukariri, huku wengine wakishindwa kabisa.

Mmoja wa wanafunzi, Kajubi Mukajanga ambaye ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), anasema Mabala alikuwa mwalimu aliyependa kuwa karibu na wanafunzi, alikuwa tayari kukaa nao nje ya darasa hata saa moja wakijadilili kuhusu mambo mbalimbali.

“Alikuwa anapenda maendeleo ya wanafunzi hadi akatusimamia kuandika mashairi ambayo yalikusanywa kwa pamoja na kuwekwa kwenye kitabu,’’ anasema.

“Kwa kifupi naweza kusema alikuwa mwalimu aliyezaliwa na kipaji cha kufundisha, kwake ilikuwa faraja kumfundisha mwanafunzi akaelewa,” alisema Kajubi, ambaye alifundishwa na Mabala katika sekondari ya Mzumbe.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii