Delcy Rodríguez ameapishwa kuwa Rais wa mpito wa Venezuela kufuatia kikao cha bunge kilichoanza kwa wito wa kutaka kuachiliwa kwa Rais aliyeelezwa kuondolewa madarakani Nicolás Maduro anayezuiliwa nchini Marekani hatua iliyozidi kuchochea mvutano wa kisiasa na kidiplomasia kati ya Caracas na Washington.
Rodríguez mwenye umri wa miaka 56 na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Venezuela tangu mwaka 2018 amesema ameumizwa na kile alichokiita “kutekwa nyara” kwa Nicolás Maduro na mkewe Cilia Flores waliokamatwa na vikosi vya Marekani katika uvamizi wa usiku wa Jumamosi.
Aidha ameeleza kuwa tukio hilo ni ukiukwaji mkubwa wa uhuru na mamlaka ya taifa la Venezuela.
Hivyo kauli hiyo imekuja saa chache baada ya matukio ya kushangaza ndani ya chumba cha mahakama jijini New York ambako Maduro alisisitiza kuwa bado ni Rais halali wa Venezuela huku akikana mashtaka manne yanayomkabili ya ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi ambayo yamefunguliwa na Marekani.
Hatua ya Marekani kumkamata Maduro imekosolewa vikali katika Umoja wa Mataifa ambapo Baraza la Usalama lilifanya kikao cha dharura kujadili hali ya Venezuela kabla ya kiongozi huyo kufikishwa mahakamani.
Balozi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa Samuel Moncada amesema nchi yake imelengwa na “shambulio haramu la silaha lisilo na uhalali wowote wa kisheria,” akisisitiza kuwa hatua ya Marekani ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Hata hivyo Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Mike Waltz amehalalisha operesheni hiyo kwa kumtaja Nicolás Maduro kama “rais haramu” na “mkwepaji wa haki,” akisisitiza kuwa Marekani haiwezi kuacha taifa lenye hifadhi kubwa zaidi ya nishati duniani kuendelea kuongozwa na kiongozi anayedaiwa kujihusisha na uhalifu wa kimataifa.
Kuapishwa kwa Delcy Rodríguez kama Rais wa mpito kunatarajiwa kuongeza mjadala wa kimataifa kuhusu uhalali wa uongozi wa Venezuela, hatma ya Nicolás Maduro na mustakabali wa kisiasa wa taifa hilo linalokabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani na shinikizo la nje.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime