Ripoti "Robo ya wateja hawana imani na malipo ya data, SMS ya Safaricom"

TAKRIBANI robo ya wateja wa Safaricom (asilimia 23) hawana imani na ada wanazotozwa kwa matumizi ya data na jumbe fupi (SMS), kulingana na utafiti wa mdhibiti wa sekta unaoangazia mienendo ya utozaji bili katika sekta ya mawasiliano nchini.

Utafiti huo unaonyesha kuwa ni asilimia 77 ya wateja wa Safaricom wanaoamini wanalipa kwa usahihi data, huku asilimia 77.7 wakisema hivyo kwa SMS.

Hii inaifanya Safaricom kusalia nyuma kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na Jamii Telecommunications, Airtel na Telkom Kenya katika uaminifu wa utozaji bili.

Jamii Telecommunications inaongoza kwa kuaminiwa zaidi, huku asilimia 98.4 ya wateja wake wakisema wanatozwa ada kwa usahihi kwa data na asilimia 88.6 kwa SMS.

Airtel inafuatia kwa asilimia 98.3 kwa data na asilimia 86.2 kwa SMS.

Kiwango hiki cha kukosa imani kwa wateja wa Safaricom kinajitokeza wakati ambapo mapato ya kampuni hiyo kutoka data yamepiku yale ya huduma za sauti kwa mara ya kwanza.

“Safaricom inaonyesha utendaji wa chini ikilinganishwa na watoa huduma wengine. Ingawa wengi bado wana imani, viwango hivi vya chini vinaonyesha kuwa wateja wa Safaricom hawana uhakika mkubwa kuhusu usahihi wa bili, hasa kwa huduma za data,” ripoti hiyo ilisema.

Mapato ya Safaricom kutoka data ya simu yaliongezeka kwa asilimia 18 hadi Sh44.4 bilioni katika nusu ya mwaka ulioishia Septemba 2025, huku mapato ya huduma za sauti yakiongezeka kwa asilimia 0.5 hadi Sh41.09 bilioni.

Utafiti huo ulifanywa na kampuni ya Strategic Synergy Consultants Limited kwa niaba ya Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) kati ya Julai 1, 2024 na Juni 30, 2025, ukihusisha zaidi ya washiriki 4,200.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa uwazi na ufafanuzi katika utozaji bili ni muhimu ili kudumisha imani ya watumiaji.

Malalamishi kuhusu bili ni miongoni mwa kesi nyingi zinazowasilishwa kwa CA kila robo mwaka.

Kwa upande wa simu za kawaida, ni asilimia 80.2 pekee ya wateja wa Safaricom wanaosema wanatozwa kwa usahihi.

Airtel inaongoza kwa asilimia 97.6, ikifuatiwa na Jamii (asilimia 96.7) na Telkom Kenya (asilimia 94).

Safaricom inaongoza sokoni kwa kuwa na asilimia 65 ya wateja wa simu nchini kufikia Septemba mwaka jana, ikifuatiwa na Airtel (asilimia 30.7), huku Telkom na Jamii kila moja ikiwa na karibu asilimia moja.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii