Ndege za Marekani zafanya ukaguzi juu anga ya Nigeria

Kulingana na uchunguzi wa shirika la habari la Reuters, ndege ya kijeshi ya Marekani imekuwa ikiruka mara kwa mara juu ya anga ya Nigeria katika wiki za hivi karibuni.

Maafisa wa Marekani wamebainisha kwa shirika la habari la Reuters kwamba hizi ni safari za ufuatiliaji na kukusanya taarifa za kijasusi, ambazo lengo lake halijafafanuliwa rasmi. Operesheni hizi ni sehemu ya muktadha mpana wa ushirikiano wa usalama ulioimarishwa, kufuatia kauli za Donald Trump zinazotishia Nigeria kuingilia kijeshi ili kuwalinda Wakristo.

Data ya ufuatiliaji wa safari za ndege katika eneo hilo inaonyesha kwamba ndege ya Marekani aina ya Gulfstream V inaondoka karibu kila siku Accra, ikiruka juu ya anga ya Nigeria, na kisha inarudi kutua Ghana. Mtindo huu umeonekana tangu Novemba 24, kulingana na uchunguzi wa Reuters, siku chache baada ya mkutano wa ngazi ya juu kati ya maafisa wa Marekani na Nigeria.

Mnamo Desemba 22, Waziri wa Habari wa Nigeria alitaja kuimarisha ushirikiano wa usalama kati ya nchi yake na Marekani, baada ya Donald Trump kutishia Nigeria kuingilia kijeshi ili kuwalinda Wakristo wa nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya kigaidi.

Mbunge wa Marekani aliyetumwa hivi karibuni kwa misheni nchini Nigeria alithibitisha kuanzishwa kwa kikosi kazi cha pamoja kushughulikia masuala ya usalama. Taarifa zilizokusanywa na shirika la habari la Reuters zinaonyesha wazi kwamba Marekani inaimarisha uwezo wake katika eneo hilo, baada ya kufunga kambi yake ya mwisho ya kijeshi huko Agadez, Niger, mnamo Agosti 2024.

Mnamo Oktoba, Donald Trump alishutumu mamlaka ya Nigeria kwa kufumbia macho kile alichodai kuwa mashambulizi yaliyolengwa dhidi ya Wakristo wa nchi hiyo.

Ndege za uchunguzi zilizogunduliwa katika wiki za hivi karibuni zinaaminika kuwa zinalenga kukusanya taarifa za kijasusi kuhusu harakati za Boko Haram na kundi la Islamic State huko Afrika Magharibi. Lengo pia litakuwa kumpata raia wa Marekani, rubani katika misheni ya kibinadamu, ambaye alitekwa nyara huko Niamey mwishoni mwa mwezi Oktoba.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii