PAPA LEO ATOA WITO WA AMANI WAKATI WA KRISMASI

Baba Mtakatifu Leo ametoa wito kwa watu wote wenye nia njema duniani kuifanya sikukuu ya Krismasi kuwa siku ya amani, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu siku hii takatifu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Akizungumza akiwa kwenye makaazi yake ya mapumziko nje kidogo ya mji wa Roma, Papa Leo amesema anarejea ombi lake la muda mrefu kwa mataifa na makundi yanayohasimiana kuweka kando tofauti zao, angalau katika kipindi hiki cha Krismasi.

Hata hivyo, Papa ameonesha masikitiko yake makubwa kufuatia taarifa kwamba Urusi imekataa kusitisha mapigano katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine, hata wakati huu wa sikukuu ya Krismasi, jambo alilolitaja kuwa kinyume na misingi ya ubinadamu na amani.

Papa Leo amesisitiza kuwa Krismasi ni wakati wa kutafakari juu ya upendo, mshikamano na matumaini, akiwahimiza viongozi wa dunia kuchukua hatua za kweli kuelekea amani ya kudumu.

Wakristo duniani kote wanatarajiwa kusherehekea sikukuu ya Krismasi kesho, wakikumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii