Maswali 7 magumu kwa Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba kutoka kwa wahariri wa vyombo vya habari kuhusu vurugu za Oktoba 29 Tanzania

Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba Novemba 25 mwaka huu alikutana na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, na maswali mazito yakielekezwa moja kwa moja kwake kuhusu kile kilichotokea Oktoba 29, 2025.

Siku hiyo ya uchaguzi na siku kadhaa zilizofuata, kulikuwa na maandamano yaliyoendana na vurugu na kusababisha vifo vya watu kadhaa, uharibifu mkubwa wa mali hasa za umma na baadhi binafsi na majeruhi. Waandamanaji wakitaka mabadiliko mbalimbali yakiwemo ya uchaguzi, haki na mifumo ya demokrasia.

Maswali hayo yaliulizwa na wahariri kutoka vyombo mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri TEF Deodatus Balile na waandishi wengine waandamizi Tanzania kama Jesse Kwayu, Caren-Tausi Mbowe, Neville Meena na Salim Kikeke, ambao walitaka majibu mahsusi kuhusu vifo, miili kutopatikana, tuhuma za kaburi la halaiki, utekaji, uhuru wa habari na madai ya hujuma za kiuchumi. Yalikuwa maswali karibu 12 aliyoulizwa Waziri Mkuu lakini haya saba yameonekana kugusa wengi.

1. Utekaji, kupotea, kubambikia kesi na taswira ya Jeshi la Polisi
Balile aliuliza hapa kwetu (Tanzania) mtu akimuona Polisi anaanza kujikagua nna bangi? Wakati mwingine hauna bangi lakini mpaka unafika kituo cha Polisi una bangi misokoto mitano kwenye mfuko, tunabadilishaje hii sura ili kuhakikisha jeshi la Polisi na kama wako watu wanaoteka wakashughulikiwe. Lingine aliuliza serikali imejipange kwamba watu hawataendelea kutekwa , kuuawa na watu hawataendelea kupotea

Majibu ya Waziri Mkuu alisema: “Hili jambo halipaswi watanzania kutufikisha kwenye kuuana, sote tunakubalina kwamba wahalifu wanatakiwa wakamatwe, tumejiwekea sheria, kama tunaona utaratibu tunaotumia umetufikisha kutoaminiana, kuleta taharuki, ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameunda tume.
Aidha kuhusu taswira ya jeshi la Polisi kwa ujumla, Waziri Mkuu alikiri kuwa kunahitajika marekebisho makubwa katika namna vyombo vya usalama vinavyofanya kazi.

“Sote tunakubaliana kwamba wahalifu wanatakiwa wakamatwe. Tatizo ni pale taratibu zetu zinapovurugika na kuleta kutoaminiana. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) ameunda tume kuangalia maeneo yenye mapungufu hasa ya uhusiano, utawala na namna ya kukamata” alisema Waziri Mkuu
Alisisitiza kuwa makosa ya mtu mmoja yasionekane kama ni sura ya Taasisi nzima;
Jinsi polisi walivyotumia nguvu kuvunja maandamano Tanzania
Mwigulu

“Tabia ya mtu mmoja ipo, lakini tusione Taasisi nzima kwa kigezo cha tukio moja.”

2. Idadi ya watu waliokufa Oktoba 29, 2025
Balile aliuliza pia kuna mjadala ni watu wangapi wamefariki? maana Aljazeera wanatuambia 700, Taasisi zingine zinasema watu 10,000 wengine wanasema 10 swali ambalo lilijaziwa na Jesse kwayu alipomuuliza Waziri Mkuu “umetueleza madhara ya yaliyotokea Oktoba 29, vituo vilivyoharibiwa, nyumba, magari mpaka pikipiki, kwanini kigugumizi kutuambia waliokufa? Mnaficha nini? Kwa sababu waliokota maiti ni polisi, utaratibu wa kupeleka maiti mochwari unajulikana, hii takwimu inafichwa ili nini?
Waziri Mkuu Mwigulu alisema mjadala wa takwimu unadhalilisha thamani ya maisha ya binadamu.
“Tukubali, vurugu hizi zimepoteza maisha ya watu. Lakini mnataka tuhesabu kama magari? Maisha ya watu mnataka tuhesabu kama magari? Hivi mnajua damu ya binadamu ilivyo?”
Akaongeza: “Watu wanaongea elfu ngapi, sijui ngapi… tusidharau uhai. Haya mambo yana madhara hata kiuchumi.”

3. Kaburi la halaiki na familia kutopatiwa miili ya ndugu zao waliofariki
Swali liliulizwa na Caren-Tausi Mbowe aliyesema “mpaka sasa hivi mtaani watu wanalalamika sana kutopata maiti za ndugu zao, kwanini hali inakuwa hivyo, sisi waandishi wa habari tumeathirika pia, mmoja wa waandishi wetu hajapatikana na wamezika nguo, sawa tumepata matatizo, madhira yametukuta, kwanini watu hawapewi maiti zao? akaongeza swali la pili kuna tuhuma kwamba kuna kaburi la halaiki, ukweli ukoje?
Katika majibu yake, Waziri Mkuu hakuzungumzia moja kwa moja kuhusu tuhuma za kaburi la halaiki.
Aliendelea kusisitiza msimamo wa serikali wa kushughulikia matukio kwa utaratibu, na kwamba Tanzania haijawahi kuwa na historia ya kufanya mambo ya aina hiyo.
Akisitiza serikali inasubiri taarifa kamili kutoka kwa mamlaka zinazochunguza matukio ya Oktoba 29.

4. Vyombo vya habari kuzibwa mdomo wakati wa uchaguzi
Waandishi wanasema walinyimwa nafasi, TCRA iliingilia kazi za uhariri, baadhi kutishwa. Neville Meena, aliuliza “Tunavyozungumza sasa hivi Waziri Mkuu, vyombo vya habari Tanzania hatuna pa kusimama, tunaonekana ni watu wa hovyo ambao hatukufanya kazi yoyote wakati wa uchaguzi, na hii ilitokana na serikali kutuminya kututisha kutokana na kile ambacho tulitaka kufanya, na hasa TCRA (Mamkala ya Mawasiliano Tanzania), kutuandikia barua na kutukataza hiki na kile, nini kauli yako kuhusiana na taasisi za serikali kutuingilia katika uhuru wetu wa kihariri na kutukataza kufanya kazi yetu ya kitaaluma inavyostahili?
Majibu ya Waziri Mkuu yalikuwa: “Kama kuna tukio, nafikiri tushughulikie na tukio husika, Tanzania iko kwenye kumbukumbu ya kutofanya mambo ya aina hiyo, na mwaka huu tu Taasisi zote za uandishi tulikuwa tunafanya tuzo, unaweza kupata tuzo kwenye nchi ambayo sio wewe unaandika, kwamba unaingiliwa kwenye uhariri? Alihoji Mwigulu na kuongeza “matukio yanaweza kujitokeza na mimi hilo sitaki tubishane nalo, ikitokea tuzishugulikie”.

5. Ushahidi wa uhujumu uchumi
Swali lililoulizwa na mwandishi wa zamani wa BBC Salim Kikeke, aliyetaka kujua kuna ushahidi gani kwamba kilichotokea kilikuwa economic sabotage? Na je, waliokamatwa ni raia wa nje?
Mwigulu alisema kiashiria kikubwa ni kulengwa kwa rasilimali na miundombinu ya wananchi.
“Tanzania si mali ya chama chochote, na rasilimali zake si mali ya mtu binafsi. Fedha zinazoathiriwa ni za wananchi. Mtu akilenga kuharibu hayo, hiyo ni economic sabotage”, akimaanisha huko ni kuhujumu na kuharibu uchumi.
Katika mkutano huo alitaja takwimu za mali zilizoharibiwa kwa kuchomwa moto wakati wa vurugu za maandamano hayo ya Oktoba 29, 2025. Ofisi za serikali 756, vituo vya mabasi ya mwendo kasi 27, mabasi 6, nyumba binafsi 273, vituo vya Polisi 159, vituo binafsi vya mafuta 672.
Pia magari ya watu binafsi 1,642 yalichomwa, pikipiki 2,268 na magari ya serikali 976 zikiwa ni takwimu za awali.

6. Nani aliyetuma kuua waandamanaji?
Swali hili liliulizwa pia na Kikeke akisema “kuna taarifa zinazungumzia vyombo vya usalama kufyatua risasi za moto hovyo hovyo, nataka kuuliza kulikuwa na order ya ‘shoot to kill’ (agizo la kufyatua risasi na kuua na kama ilikuwepo ilikuwa imetolewa na nani?
Waziri Mkuu alijibu kwa kuhoji “Pakitokea vurugu, unarudi lini kuuliza kwamba nishoot ama nisishoot? Na tunaona idadi kubwa ya askari wamepoteza Maisha yao, nani kaweka order (kaagiza) wapigwe risasi? Hili ni jambo baya limeshatokeatusubiri tupewe ukweli wake, ukitaka tupewe aliyetoa, aliye-shoot askari (agizo hilo) order hiyo alipokea wapi?

7. Vuguvugu la Disemba 9, Tanzania imejiandaa vipi?
Swali lingine la Kikeke lilihusu kinachoendelea mitandano kwamba kuna maandamano mengine yanaandaliwa yatakayofanyika Disemba 09 mwaka huu na je, serikali imejipangaje?
Waziri Mkuu alijibu kwa kutoa wito wa kutotengeneza mzunguko mwingine na mpya wa vurugu zingine.
“Rai yangu kwa watzania wotemenye dukuduku , kero yoyote ile tujitenge na tuambizane tukatae kwenda tena kwenye mambo ya aina hiyo, tumbakize adui pekee anayemezea mate rasilimali za nchi yetu”
Aliongeza: “Lakini hata anayeandaa maandamano hii siyo wakati mzuri, watu wanaomboleza wapendwa wao, si jambo zuri, wale wanaohamasisha kupitia mitandao ni kwa sababu wao na jamaa zao wote wako huko (nje), laiti angeguswa na jambo hili hangemwambia mtu fanya hivi, wanafanya hivi kwa sababu wao na jamaa zao wote wako kule na wengine nadhana washapata na uraia wa nchi zingine”

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii