Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imewahakikishia wakazi wa Mkolani, Nyegezi na maeneo ya jirani kuwa upatikanaji wa maji safi na salama utaboreshwa na kuwa wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji.
Akizungumza na Jembe FM, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa MWAUWASA, Bi. Vivian Temu, amesema mamlaka hiyo inaendelea na ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhi maji katika eneo la Nyamazombe, ambalo litahudumia maeneo ya Mkolani, Nyegezi na vitongoji vya karibu.
Aidha, Bi. Vivian amesema MWAUWASA inatekeleza mradi wa ujenzi wa matanki matano katika maeneo ya Sawa, Kisesa, Fumagila, Usagara na Nyamazombe, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha maji yanawafikia wananchi baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa chanzo cha maji cha Butimba.
“Tunaamini kuwa mradi huu wa Ujenzi wa matanki utakuwa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji katika maeneo Mbalimbali ya jijini la mwanza. Dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani inaendelea kutekelezwa. Ni muhimu Wananchii kuwa na uvumilivu ili mradi ukamilike kwa ubora, kwa wakati na kuleta tija,” amesema Bi Vivian
Amesisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji kwa ajili ya matumizi ya sasa na baadaye, ili kuzuia uharibifu na kuongeza ufanisi wa huduma.
Bi. Vivian amewataka wananchi kutoa taarifa haraka kwa mamlaka hiyo endapo kutatokea changamoto yoyote, ili hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu.
Na @MustaphaKinkulah
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime