Rais wa Guinea-Bissau akamatwa na wanajeshi baada ya uchaguzi wenye utata

Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embaló, amekamatwa na wanajeshi wenye silaha leo Jumatano zikiwa zimepita siku tatu baada ya uchaguzi wa Rais ulioandaliwa kwa hali iliyojaa utata na migogoro ya kisiasa.

Mashuhuda wamesema milio ya risasi ilisikika karibu na Ikulu ya Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani na Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE), huku wanajeshi wakidhibiti maeneo muhimu ya serikali katika mji mkuu, Bissau.

Taarifa zinadai kuwa pamoja na Embaló, wengine  waliokamatwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Majeshi na naibu wake wakipelekwa sehemu isiyojulikana.

Uchaguzi wa rais uliofanyika  Novemba 23 mwaka huu  ulikumbwa na utata mkubwa baada ya mgombea wa upinzani, Fernando Dias da Costa kudai ushindi, huku siku moja baadaye, Rais Embaló naye alitangaza kwamba ameshinda, hali iliyochochea mvutano na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa.

Tume ya Uchaguzi haikutangaza matokeo rasmi na duru za kisiasa zilidai kuwa kulikuwa na shinikizo, madai ya wizi wa kura, pamoja na kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea wakuu wa upinzani.

Tangu kupata uhuru wake mwaka 1973, Guinea-Bissau imewahi kushuhudia zaidi ya mapinduzi manne ya kijeshi, wataalamu wa siasa za Afrika Magharibi wanaonya kwamba tukio hili linaweza kurudisha nyuma juhudi za kidemokrasia na kuichimbia nchi kwenye mkwamo wa kisiasa na kiusalama.

Na@ MustaphaKinkulah

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii