Tanzania na Estonia kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kidijitali

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Estonia zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali zenye maslahi mapana kwa nchi hizi mbili ikiwemo maendeleo na mageuzi ya tekolojia ya kidijitali, ubunifu katika elimu, usalama wa mtandao na fursa za kibiashara na uwekezaji.

 Hayo yamebainishwa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Zanzibar, Mhe. Shariff Ali Shariff na Waziri wa  Sheria na masuala ya Kidigitali wa Estonia, Mhe. Liisa Pakosta yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya unaendelea jijini Luanda, Angola.

 Wakati wa mazungumzo hayo ambayo yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Estonia, Mhe. Shariff aliishukuru Serikali ya Estonia kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania hususan katika kuunga mkono jitihada zake katika mageuzi ya kidijiti ambapo pia alitumia fursa hiyo kumhakikishia ushirikiano kutoka Tanzania katika sekta nyingine zenye maslahi mapana baina ya nchi hizi mbili ikiwemo biashara na uwekezaji.

 Kwa upande wake, Mhe. Pakosta alieleza kuwa Estonia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika mageuzi na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali na kutambulisha maeneo mapya ya ushirikiano hususan mpango wa AI Leap unaotekelezwa katika shule za Estonia. 

 Aliongeza kwa kusema  kuwa ushirikiano wa pande mbili  baina ya Tanzania na Estonia umekuwa thabiti kwa muda mrefu na kueleza kuridhishwa na hamasa ya Tanzania katika masuala ya kidijitali.

Aidha alibainisha kuwa, katika ziara ya hivi karibuni nchini Tanzania, ujumbe wa Estonia ulivutiwa na maendeleo ya programu za kidijitali za Tanzania zinazoendana vizuri na mfumo wa Estonia na kwamba  idadi kubwa ya ujumbe wa Watanzania wanaotembelea Estonia kwa mafunzo na kubadilishana uzoefu ni  ishara ya kuimarika kwa  ushirikiano huo.

Hata hivyo Mhe. Pakosta alisisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kushirikiana katika usalama wa mtandao, huku akieleza kuwa nchi yake imezindua programu mpya chini ya shirika lake la maendeleo la ESTDEV ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi za kipaumbele zilizojumuishwa kwenye mpango huo

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii