Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt amesema Donald Trump "amechoshwa na mikutano ya mara kwa mara" ambayo hadi sasa haijatoa mwanga wa kufikiwa kwa makubaliano ya kuvimaliza vita kati ya Urusi na Ukraine.
Ametoa kauli hiyo wakati Kyiv ikieleza kwamba Washington bado inaishinikiza ikubali mpango wake unaojumuisha kuachia baadhi ya maeneo yake kwa Urusi kama sehemu ya makubaliano ya kuvimaliza vita vilivyodumu takriban miaka minne.
Leavitt amewaambia waandishi wa habari kwamba Trump hataki tena kile alichokiita maneno matupu bila vitendo na kwamba anachotaka kuona sasa ni vita hivyo kufika mwisho.
Hata hivyo hivi karibuni Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitoa kauli iliyoashiria kwamba hakuna mabadiliko makubwa katika msimamo wa Marekani juu ya namna vita hivyo vinapaswa kumalizika tangu Washington ilipowasilisha mpango wake wa vipengele 28 mwezi uliopita - mpango ulioonekana kuipendelea zaidi Urusi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime