Mkoa wa Katavi umeendelea kuwa kivutio cha wawekezaji kufuatia maboresho makubwa ya miundombinu, usalama na kasi ya utoaji leseni katika Sekta ya Madini.
Afisa Madini Mkazi wa mkoa huo, Mhandisi Andrew Mwalugaja, ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa zinazopatikana katika dhahabu, shaba, risasi, fedha, nikeli, manganese na madini ya ujenzi.
Amesema kuwa ofisi yake imeongeza kasi ya utoaji leseni, ikiwemo leseni tatu za utafiti na zaidi ya leseni 300 za uchimbaji mdogo na wa kati ndani ya miezi minne. Katika biashara ya madini, leseni 82 tayari zimetolewa kati ya Julai na Oktoba mwaka huu hatua inayodhihirisha mwamko mkubwa wa uwekezaji.
Serikali imeanzisha masoko mawili ya madini Mpanda na Karema ili kuhakikisha wachimbaji, hususan vijana, wanapata soko la uhakika na kufanya shughuli zao kwa uwazi zaidi. Hadi sasa, mkoa umefanikiwa kuongeza makusanyo ya maduhuli hadi Shilingi bilioni 3.80 ndani ya miezi minne tu.
Wachimbaji na wawekezaji wamesema maboresho ya mazingira ya uwekezaji, matumizi ya teknolojia za kisasa na ushirikiano mzuri na Serikali yameongeza uzalishaji, ajira na mapato ya Serikali. Kampuni ya Jiuxing Tanzania Mining Company imeeleza kuwa ushirikiano na wataalam pamoja na teknolojia ya froth flotation umeongeza tija, usalama na ujuzi kwa vijana wa Mpanda.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime