Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini Cameroon limetoa wito wa utulivu huku kukiwa na hofu ya kutokea machafuko wakati nchi hiyo ikisubiri matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 12.
Mgombea wa upinzani na msemaji wa zamani wa serikali Issa Tchiroma Bakary amejitangaza mshindi, akidai kuwa amemshinda Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 92, anayetaka kurefusha utawala wake wa miaka 43 kwa miaka mingine saba.
Kujitangaza kwa Tchiroma kumeibua shutuma kali kutoka kwa serikali na chama tawala cha Biya cha Cameroon People's Democratic Movement (CPDM), huku maafisa kadhaa wakipuuzilia mbali kuwa ni kinyume cha sheria na bado ni mapema.
Baraza la Katiba bado halijatangaza matokeo ya mwisho na lina hadi Oktoba 27 kutangaza rasmi mshindi. Kukaidi na kusisitiza kwa Tchiroma kwamba "atatetea ushindi wake" kumeongeza wasiwasi kwamba kutangazwa kwa matokeo kunaweza kusababisha ghasia au machafuko katika taifa hilo la Afrika ya Kati.
Katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Maaskofu la Cameroon (NECC), maaskofu wa Kikatoliki wa nchi hiyo wamehimiza kujizuia na kuomba amani na utulivu. "Tunatumai kwamba matokeo rasmi yataakisi mapenzi ya wapiga kura, na kwamba hakuna kitakachobadilishwa na mamlaka yoyote inayohusika katika mchakato huu," maaskofu wamesema.
Kanisa Katoliki, mojawapo ya taasisi zinazoheshimika zaidi nchini Cameroon, linaonekana kwa wingi kuwa sauti ya kimaadili katika masuala ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo. Wito wake wa utulivu unaangazia wito unaoongezeka kutoka kwa mashirika ya kiraia na waangalizi wa kimataifa kwa ajili ya uwazi na haki katika mchakato wa uchaguzi.
Baadhi ya makasisi hapo awali walikosoa utawala wa muda mrefu wa Rais Biya na rekodi ya utawala. Mnamo wezi Januari, Askofu Yaouda Hourgo, Askofu wa Yagoua katika Mkoa wa Mbali Kaskazini, alisema wakati wa mahubiri kwamba "ingekuwa vyema kwa shetani kuchukua mamlaka" kuliko Paul Biya kugombea tena, akitaja mateso ya watu wa kawaida wa Cameroon.
"Hatutateseka zaidi ya haya tuliyoshuhudia. Tayari tumeteseka vya kutosha," Askofu Hourgo alisema.
Kufuatia maandamano ya upinzani kuhusu madai ya udanganyifu katika uchaguzi, Baraza la Katiba lilitangaza kuwa litaanza kusikiliza malalamiko siku ya Jumatano. Uamuzi wake utakuwa muhimu katika kuamua kiongozi ajaye wa nchi.