Rais wa zamani wa Ufaransa Sarkozy anaanza kutumikia kifungo cha miaka mitano jela

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy atawekwa rumande leo Jumanne. Ataanza kifungo cha miaka mitano jela kwa kula njama ya kukusanya fedha za kampeni nchini Libya. Ni pigo kubwa kwa kiongozi huyo aliye jizolea sifa na mashuhuri wa kimataifa.

Sarkozy, rais wa kihafidhina wa Ufaransa kuanzia mwaka 2007 hadi 2012, atakuwa kiongozi wa kwanza wa Ufaransa kufungwa tangu mshirikishi wa Nazi Marshal Philippe Pétain baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

"Siogopi jela. Nitatii, hata kwenye lango la gereza," Sarkozy ameliambia Gazeti la La Tribune Dimanche kabla ya kufungwa kwake.

Hukumu hii inahitimisha miaka mingi ya vita vya kisheria vinavyohusu madai kwamba kampeni yake ya mwaka 2007 ilifuja mamilioni ya dola kutoka kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, ambaye alipinduliwa na kuuawa wakati wa maasi ya Arab Spring.

Ingawa Sarkozy alipatikana na hatia ya kula njama na washirika wake wa karibu kuandaa mpango huo, alifutiwa mashtaka ya kupokea au kutumia pesa hizo kibinafsi.

Amekuwa akikana kosa lolote na kuitaja kesi hiyo kuwa ya kisiasa, akidai majaji walikuwa wakitaka kumdhalilisha. Amekata rufaa, lakini aina ya hukumu yake inamtaka abaki gerezani kwa muda wote wa rufaa yake.

Rais huyo wa zamani tayari ametiwa hatiani katika kesi nyingine ya rushwa, ambapo alipatikana na hatia ya kujaribu kupata taarifa za siri kutoka kwa jaji ili kupata upendeleo wa kitaaluma, akitumikia kifungo chake akiwa amevalia bangili ya kielektroniki kwenye kifundo cha mguuni.

Katika gereza la La Santé mjini Paris, ambalo hapo awali alifungwa mwanaharakati wa mrengo wa kushoto Carlos le Chacal na kiongozi wa Panama Manuel Noriega, Sarkozy huenda akazuiliwa katika kitengo cha kifungo cha upweke, ambapo wafungwa huwekwa katika vyumba vya watu binafsi na kutengwa wakati wa shughuli za nje kwa sababu za usalama.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii