Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kukutana na Vladimir Putin na Donald Trump mjini Budapest iwapo ataalikwa kwenye mkutano kati ya viongozi wa Urusi na Marekani. Mkutano huu, ulioandaliwa na Trump kujadili amani nchini Ukraine, unaweza kufanyika baada ya wiki chache. Hata hivyo, Zelensky amesema kuwa Ukraine inajiandaa kununua mifumo 25 ya ulinzi wa anga ya Patriot.
Rais Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Marekani Donald Trump katika mkutano wao wa kilele nchini Hungary iwapo ataalikwa.
Trump na Putin walitangaza mkutano wao katika mji mkuu wa Hungary, yumkini ndani ya wiki chache, wakati rais wa Marekani anaendelea kujaribu kujadili makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya miaka mitatu na nusu, vilivyochochewa na mashambulizi kamili ya Urusi mnamo mwaka 2022.
Rais wa Ukraine alikosoa uchaguzi wa Hungary, ambayo ina uhusiano mbaya na Kyiv na inachukuliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya anayeunga mkono zaidi Kremlin.
"Siamini kwamba waziri mkuu ambaye anazuia Ukraine kila mahali anaweza kuleta chochote chanya kwa Waukraine, au hata mchango wa uwiano," Zelensky amesema, akimaanisha kiongozi wa Hungary Viktor Orban.
Kyiv imeeleza nia yake ya kushiriki katika mkutano wa pande tatu kati ya Zelensky, Putin, na Trump katika nchi kadhaa zisizoegemea upande wowote, zikiwemo Uturuki, Uswisi na Vatican.
Mnamo mwaka 1994, Moscow ilitia saini mkataba huko Budapest uliolenga kuhakikisha usalama wa Ukraine, Belarus, na Kazakhstan badala ya kutelekezwa kwa silaha nyingi za nyuklia za enzi ya Soviet.
Tangu arejee Ikulu ya White House mapema mwaka huu, Trump amelenga kumaliza haraka mzozo wa miaka mingi nchini Ukraine. Alihimiza mfululizo wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya maafisa wa Ukraine na Urusi na akawa mwenyeji wa Putin kwa mkutano wa kilele huko Alaska-juhudi za kidiplomasia ambazo hazikuzaa matunda yoyote.
Wkati huo huo katika tangazo tofauti, Zelensky amesema nchi yake inatayarisha kandarasi ya kununua mifumo 25 ya ulinzi wa anga ya Patriot.
Ununuzi huo ungeimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa Ukraine wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya anga ya Urusi.
Akizungumza na vyombo vya habari katika mkutano wa Jumapili, Zelensky alisema mifumo hiyo itatolewa kila mwaka kwa miaka kadhaa na kwamba Ukraine itatafuta kipaumbele kutoka kwa baadhi ya nchi za Ulaya kwa ajili ya kupata mifumo hiyo.