Niffer na wenzake 21 wasomewa mashtaka matatu ya uhaini

Mfanyabiashara Jeniffer Jovin Bilikwija maarufu ‘Niffer’ na wenzake 21 wamesomewa mashtaka matatu ya uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.

Niffer (26) na wenzake hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya na Jopo la Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Hemed Khalfan.

Katika shtaka la kwanza linawakabili Watuhumiwa wote 22 akiwemo Niffer ambapo wanadaiwa kati ya Oktoba 1 hadi 29 mwaka huu katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ubungo, Dar es salaam walipanga njama ya kutenda kosa la uhaini.

Kosa la pili linawakabili Watuhumiwa 21 isipokuwa Niffer ambapo wakidaiwa kuanzisha nia ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa lengo la kuitishia mamlaka na wakatekeleza nia hiyo kwa kusababisha uharibifu wa mali za Serikali.

Kosa la tatu la uhaini ambalo linamkabili Niffer peke yake akidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 1 mpaka Oktoba 24 mwaka huu maeneo mbalimbali ya Dar es salaam akiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alianzisha nia ya kuvuruga ama kuzuia uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 la lengo la kuitishia mamlaka kuu na alitekeleza nia hiyo kaa kuhamasisha umma kununua Barakoa za kuzuia mabomu ya machozi ambapo alihamasisha zinunuliwe kutoka kwenye biashara yake ili Watu wanunue kujikinga katika maandamano hayo ya kuvuruga uchaguzi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Lyamuya aliwaambia Washtakiwa wote kwamba hawapaswi kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Baada ya kueleza hayo Wakili Kibatala aliomba maombi kadhaa kwa Mahakama hiyo ikiwemo ombi la Mahakama itoe amri kwa Magereza ya kwamba Washtakiwa hao wapatiwe matibabu akiwemo Niffer ambaye alifanyiwa vitendo vya ukatili kwa kupigwa na Maafisa kadhaa wa Polisi ambao walilazimisha asaini maelezo yanayosemekana kuwa ni ya onyo.

Hata hivyo Hakimu Lyamuya alitupilia mbali maombi hayo huku akikubaliana na ombi la Washtakiwa kupatiwa matibabu,Kesi imeahirishwa Novemba 11 mwaka huu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii