Wanane wateuliwa Zanzibar kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameteua wanane kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwemo wawili waliokatwa majina yao na kamati za uteuzi za Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa mchakato wa kuwapata wagombea.

Miongoni mwa walioteuliwa ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustapha.

Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari usiku huu wa jana Alhamis Novemba 6 mwaka huu ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Zena Said uteuzi huo umeanza jana.

Wengine walioteuliwa ni Masoud Ali Mohamed ambaye alikuwa mwakilishi wa Ole na Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye jina lake lilikatwa katika mchakato wa uteuzi wa ndani ya chama.

Mwingine ambaye alishindwa katika kura za maoni za CCM lakini kateuliwa na Rais ni Nadir Abdulatif ambaye kipindi kilichopita alikuwa mwakilishi wa Kijini na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.

Taarifa hiyo imemtaja pia Tawfiq Salim Turky ambaye alikuwa Mbunge wa Mpendae lakini na yeye jina lake lilikatwa na vikao vya CCM vya uteuzi wakati wa mchakato wa kugombea katika uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka huu.

Aliyeteuliwa mwingine Shariff Ali Shariff ambaye katika kipindi kilichopita pia aliteuliwa kuwa mwakilishi na kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii