Wanaogushi akaunti za jeshi mitandaoni waonywa vikali

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetoa onyo kali kwa watu wanaogushi akaunti za jeshi hilo na kuzitumia kinyume na taratibu, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya JKT jijini Dodoma imeeleza kuwa kumekuwepo na watu wanaotumia nembo na rangi za jeshi hilo kuunda akaunti bandia na kusambaza taarifa zisizo sahihi, jambo linalosababisha taharuki miongoni mwa wananchi.

“Wananchi tunawasihi muwe makini na taarifa zinazotolewa kiholela mitandaoni, kwani nyingi si za kweli na zinalenga kupotosha jamii. Mnapokutana na taarifa za aina hiyo, zipeni taarifa kwa mamlaka husika badala ya kuzisambaza,” imesema taarifa hiyo.

Jeshi hilo limesema halitowavumilia watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, na limewataka wanaofanya uhalifu huo kuacha mara moja kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Aidha JKT imebainisha kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini na kuwakamata wote wanaohusika na uundaji wa akaunti hizo bandia, na kwamba watakaothibitika watafikishwa katika vyombo vya sheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii