Mgombea urais SAU Majaliwa Kyara ataja vipaumbele vitatu

Mgombea urais kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majaliwa Kyara, amesema mojawapo ya vipaumbele vyake endapo atachaguliwa kuongoza nchi ni kusimamia kwa dhati sekta za kilimo, viwanda na teknolojia ili kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 16 mwaka huu katika viwanja vya Manyema, Manispaa ya Moshi, Kyara alisema sekta hizi ni nguzo kuu za uchumi wa taifa, na ukiboresha, zinaweza kuongeza ajira, kipato cha wananchi, na mapato ya Serikali.

Aliongeza kuwa serikali yake itaunda mazingira rafiki kwa wakulima wadogo na wa kati ili kuongeza tija na uzalishaji, sambamba na kufanikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo.

Aidha, ameeleza kuwa matatizo ya ajira kwa vijana yamesababishwa na mfumo wa elimu usiozingatia ujuzi wa kujitegemea, hivyo ametaka marekebisho ya mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda.

Majaliwa pia aliwatahadharisha wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 29 mwaka huu ili aweze kufanikisha mpango wake wa kuanzisha viwanda vitakavyoongeza ajira, kukuza uchumi wa taifa na kuboresha ustawi wa wananchi wote.

Kwa upande mwingine, mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi, Isack, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuwatumikia wananchi, atahakikisha mji wa Moshi unapendezesha mazingira yake kwa kupanda miti na matunda, kupandisha mishahara ya watumishi wa umma ambapo kima cha chini kitakuwa Shilingi milioni moja, pamoja na kutatua tatizo la ajira kwa vijana.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii