Polisi Shinyanga yawahakikisha amani wananchi kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 29

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga limewahakikishia wananchi wa mkoa huo kuwa kutakuwepo na amani ya kutosha siku ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu  na kuwataka wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi, ametoa kauli hiyo leo Oktoba 18 mwaka huu  wakati akizungumza na madereva wa bajaji, bodaboda na magari madogo (haice) katika Soko Kuu la mjini Shinyanga.

Amesema Jeshi hilo lipo kamili kulinda Amani siku ya Uchaguzi Mkuu, na kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi, bali wajitokeze kwa wingi kupiga kura, na kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka ambao watawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga tumejipanga vyema kuhakikisha amani inaendelea kutawala siku zote na siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu tunawaomba wananchi wote wajitokeze kwenda kupiga kura sababu amani itakuwepo na hakutakuwa na vurugu zozote,”amesema Magomi.

Aidha amewaonya watu au baadhi ya vikundi kama wapo ambao wamepanga kufanya vurugu siku ya uchaguzi, kwamba wasije kuthubutu, sababu wamejipanga vyema kudhibiti fujo na kusisitiza  jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao.

Naye Mwenyekiti wa Boda Boda Manispaa ya Shinyanga Juma Mrabu, amesema vijana wa bodaboda hawapo tayari kutumika kuvuruga amani ya nchi siku ya Uchaguzi Mkuu,bali watashiriki kwenda kupiga kura na kurudi kuendelea na shughuli zao kama kawaida za kujitafutia kipato.

Oktoba 29 ni siku ya kupiga kura ya kuchagua Rais,Wabunge na Madiwani ambao wataongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo hadi 2030.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii